Na: Hughes Dugilo, DAR ES SALAAM.
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimevunja rekodi na kuwa chuo cha kwanza kwa udahili wa wanafunzi wengi wanaotaka kujiunga na Chuo hicho katika kipindi cha wiki moja cha maonesho ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yaliyomalizika Julai 31,2021 Jijini Dar es Salaam.
Katika maonesho hayo licha ya Chuo hicho kikongwe nchini kufanya udahili wa papo hapo kwenye kozi mbalimbali, pia kilitambulisha kozi mpya ya Rasilimali za nyuki na Asali inayotolewa kwenye ndaki ya Katavi ambapo ilionekana kuvutia wanafunzi wengi kwenye maonyesho hayo.
Anitha Ngesi ni Ofisa Udahiiri Ndaki ya Mizengo Pinda iliyopo mkoani Katavi inayotoa kozi hiyo ameeleza jinsi ambavyo wanafunzi walivyovutiwa nayo na kujitokeza kuomba kujiunga nakwamba mpaka sasa wameweza kuvuka lengo kwa kudahili idadi kubwa ya wanafunzi tofauti na malengo ya idadi waliyoitaka awali.
“Kwakweli zoezi limekwenda vizuri na tumepata wanafunzi wengi ambao wamefika hapa kuomba kujiunga na tumewasaidia pia na wazazi wengine ambao watoto wao wako jeshini pia wamefika na details zao tumewasaidia kuwadahili hivyo zoezi limeenda vizuli kwa ujumla” Amesema Anitha.
Ameongeza kuwa kwa upande wa kozi ya Nyuki imewahamasisha wazazi wengi na Vijana mbalimbali wanaotaka kujiunga kwenye chuo chao nakwamba wameweza kuvuka lengo la idadi waliyoitaka.
“Nataka niwaeleze kuwa matokeo ni mazuri sana na watu wameielewa sana, kwanza nyuki kwa sasa ni kilimo ambacho kina tija kubwa sana sababu nchi nyingi zimekuwa zikihitaji Asali kutoka Tanzania ambayo ina ubora hivyo tumewaeleza hii fursa na wameweza kuipokea” Ameongeza Anitha.
Kwa upande wake Mhadhiri wa Chuo hicho Dkt. Innocent Babili amesema kuwa wamefarijika sana kuona mwitikio umekuwa mkubwa kwa waombaji wa kozi yao mpya ya Rasilimali nyuki ambayo imevuka kiwango cha idadi ya wanafunzi waliohitajika.
“Unajua siku hizi maswala ya Rasilimali nyuki pamoja na mazira yenyewe ambayo hao nyuki wanapatikana yamekuwa mambo muhimu sana unapotaka kuzalisha Asali inatakiwa kuwepo mazingira rafiki na salama kwa hiyo hii degree ya nyuki ni muhimu sana kwani inajumisha utunzaji wa mazingira kwa ujumla” Alisema Dkt. Babili.
Mhadhiri msaidizi (SUA) Hekima Mliga akizungumzia kuhusu udahili wa wanafunzi kwa ujumla amesema kuwa kumekuwa na muitikio mkubwa kwa waombaji wa kike ambo ni zaidi ya nusu ya waombaji wote waliojitokeza kufanya udahili wa papo hapo kwenye Maonesho ya Elimu ya Juu yaliyomalizika hivi karibuni Jijini Dar es Salaam.
Amefafanua kuwa “japokuwa bado zoezi la udahili linaendelea lakini mpaka sasa asilimia 52 (52%) ya waombaji wote ni jinsia ya kike ambao ni kama nusu ya waombaji wote waliopata udahili ambapo wavulana ni asilimia 48 (48%) ya waombaji” Akifafanua.
“Kwangu najisikia furaha sana kuona muitikio mkubwa kwa watoto wa kike kujiunga na masomo ya sayansi na kilimo kwa kuzingatia kilimo siku hizi kimepiga hatua hivyo kuwepo kwa idadii kubwa ya watoto wetu wa kike kutaka kusoma masomo haya kunaonesha kuhamasika kwa jamii yetu hasa kwa Wanawake”. Amesisitiza.
Mwisho