Home KIDSNEWS WAREMBO WA MISS TANZANIA WAKABIDHI MAKTABA YA WATOTO WANAOSUMBULIWA NA MARADHI YA...

WAREMBO WA MISS TANZANIA WAKABIDHI MAKTABA YA WATOTO WANAOSUMBULIWA NA MARADHI YA MOYO NA SARATANI

Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Doroth Gwajima akionesha baadhi ya vitabu vinavyopatikana katika maktaba mpya ya watoto wanaolazwa hospitali kwa muda mrefu baada ya kuzindua maktaba hiyo iliyotengenezwa  na Ubalozi wa Ufaransa pamoja na Taasisi  ya Beauty Legacy leo Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania Mhe. Fr’ediric Clavier na katikati ni Mwanzilishi wa Taasisi ya Beauty Legacy Miss Jacqueline Mengi.
Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Doroth Gwajima akiwaangalia watoto waliolazwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wanavyosoma vitabu katika maktaba mpya ya watoto wanaolazwa hospitali kwa muda mrefu baada ya kuzindua maktaba hiyo iliyotengenezwa na Ubalozi wa Ufaransa pamoja na Taasisi  ya Beauty Legacy leo Jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania Mhe. Fr’ediric Clavier.  
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Doroth Gwajima akizungumza na Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania Mhe. Fr’ederic Clavier na mwanzilishi wa Taasisi ya Beauty Legacy Miss Jacqueline Ntuyabaliwe Mengi kabla ya kuzindua maktaba ya watoto wanaolazwa hospitali kwa muda mrefu wakati wa uzinduzi wa maktaba hiyo uliofanyika katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) leo Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Doroth Gwajima akikata utepe kuashiria uzinduzi wa maktaba mpya ya watoto wanaolazwa hospitali kwa muda mrefu iliyotengenezwa na Taasisi ya Beauty Legacy pamoja na Ubalozi wa Ufaransa leo wakati wa uzinduzi huo uliofanyika katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya watoto waliolazwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa ajili ya kupatiwa matibabu ya magonjwa ya moyo na wenzao kutoka hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa ajili ya kupatiwa matibabu ya Saratani wakisoma vitabu katika maktaba mpya ya watoto wanaolazwa hospitali kwa muda mrefu baada ya kuzinduliwa kwa maktaba hiyo iliyodhaminiwa na Ubalozi wa Ufaransa pamoja na Taasisi ya Beauty Legacy leo Jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Doroth Gwajima akiwa katika picha ya pamoja na watoto waliolazwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa ajili ya kupatiwa matibabu ya moyo baada ya kuzindua maktaba mpya ya watoto wanaolazwa hospitali kwa muda mrefu iliyotengenezwa na  Ubalozi wa Ufaransa kwa kushirikiana  na Taasisi ya  Beauty Legacy leo Jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Prof. Mohamed Janabi na wanne kutoka kushoto ni Mwanzilishi wa Taasisi ya Beauty Legacy Miss Jacqueline Ntuyabaliwe Mengi

Picha na: JKCI

Na: Mwandishi Maalum –  Dar es Salaam

09/07/2021 Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Doroth Gwajima ameziomba sekta binafsi kuwekeza katika sekta ya afya ikiwa ni pamoja na kujenga maktaba za watoto katika Hospitali na vituo vya Umma vya kulelea watoto ambazo zitawasaidia kujisomea, kuwajenga kisaikolojia na kuimarisha akili zao wakati wakipatiwa matibabu.

Waziri Dkt. Gwajima ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akizindua maktaba ya watoto wanaosumbuliwa na maradhi ya Moyo na saratani wanaotibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

Dkt. Gwajima alisema yuko tayari kushirikiana na sekta binafsi ili sekta ya afya iweze kwenda mbele zaidi, jambo la muhimu ni kwa wadau hao kufuata sheria na kanuni zilizopo.

“Leo hii nimezindua maktaba ya watoto wanaotibiwa katika Hospitali za JKCI na MNH lakini kuna watoto wanatibiwa katika Hospitali  ya Saratani Ocean road na Hospitali tano za kanda ambazo ni Bugando, Mbeya, KCMC, Benjamini Mkapa na vituo vyetu vya malezi , katika hospitali hizi kuna watoto ambao kutokana na maradhi yao wanakaa hospitalini muda mrefu wakipata matibabu”,.

“Ninawaomba wadau wa sekta binafsi mjitokeze kujenga maktaba za watoto katika Hospitali hizi, kwani mtoto wakati anapata matibabu au akiwa anasubiri matibabu yake akipata vitabu vya kujisomea vitamfariji  na  kumjenga kisaikolojia kuwa ingawa anaumwa lakini anapata elimu kama wanavyopata watoto wengine”, alisema Dkt. Gwajima.

Dkt. Gwajima aliwashukuru warembo waliowahi kushinda taji la Miss Tanzania miaka mbalimbali wakiongoza na Miss Tanzania wa mwaka 2000, Jacqueline Ntuyabaliwe Mengi kwa moyo wao wa upendo na kuona umuhimu wa kujenga maktaba na kuweka vitabu ili kuwasaidia watoto waliolazwa Hospitalini muda mrefu kwa ajili ya matibabu.

“Ninawashukuru sana kwa huduma hii mliyoitoa kwa watoto wetu, pamoja na kushiriki katika mashindano ya urembo nyinyi pia ni kina mama mmeguswa na kuamua kuwasaidia wahitaji. Watoto hawa wakati wanapata matibabu  wanakosa muda wa kwenda shule na hivyo kuwa nyuma kimasomo ukilinganisha na wenzao wanaokwenda shule muda wote lakini kwa  vitabu hivi mlivyovitoa watapata muda wa kujisomea”, alishukuru Waziri Dkt. Gwajima.

Kwa upande wake kiongozi wa warembo hao (Beauty legacy) Miss Tanzania mwaka 2000 Jacqueline Ntuyabaliwe Mengi  alisema ndoto ya kujenga maktaba hiyo aliipata mwaka jana alipokuwa anatimiza miaka 20 tangu aliposhinda taji hilo kwa kushirikiana na wenzake wakaona ni vyema kutengeneza maktaba hiyo ili kuisaidia jamii.

Jacqueline alisema mamiss hao kila mtu anafanya kazi yake wakaona ni vyema  waunganishe nguvu zao kwa pamoja ambapo mwaka jana waliandaa ‘gala dinner’ na kuchangisha fedha ambazo zimewasaidia kujenga  maktaba ya watoto pia wamekusanya vifaa vya watoto wanaozaliwa  kabla ya kutimiza umri “njiti” ambavyo watavikabidhi hivi karibuni katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

“Kuna watoto ambao wanakaa Hospitalini muda mrefu hawaendi shule tumenunua vitabu vya mitaala ambavyo wanasoma shuleni, tunaamini vitabu hivi vitaleta faraja kwao. Maktaba iko wazi kwa yeyote ambaye ataona anavitabu alete kwa ajili ya watoto hawa ili waweze kujisomea”, alisema Jacqueline.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi alisema Taasisi hiyo itaajiri mwalimu mmoja na mkutubi mmoja kwa ajili ya kuwasaidia watoto hao waweze kusoma vitabu hivyo na kuvielewa.

Alisema kuwepo kwa vitabu hivyo ambavyo vitawafanya watoto wasome hadithi mbalimbali pamoja na masomo yao ya darasani ni sehemu ya tiba kwao ambayo itawajenga kisaikolojia na kuamini kuwa baada ya kupona watarudi shuleni na kuendelea na masomo yao kama kawaida.

Naye Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania Mhe. Fr’ederic Clavier ambaye Ubalozi wake umesaidia katika ujenzi wa maktaba hiyo alisema kuwepo kwa maktaba ya watoto katika Hospitali  kunatoa faraja kwa familia na watoto ambao wako katika maumivu ya magonjwa ya moyo na saratani.

“Iwapo jamii nzima itaungana kwa pamoja sioni sababu ni kwa nini mtoto anakufa leo kwa magonjwa ya moyo na saratani, kuna haja ya kuungana kwa pamoja ili kupunguza hatari ya kupata magonjwa haya  katika familia kwa kufanya hivyo tutaokoa maisha ya watu na kutoa moyo kwa familia zenye watoto wagonjwa”, alisisitiza Balozi Clavier.

Mwishoni mwa mwaka jana warembo hao walitembelea Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa ajili ya kuwasilisha wazo lao la kujenga maktaba kwa ajili ya watoto wanaougua maradhi ya saratani, moyo pamoja na maradhi mengine yanayowafanya wakae Hospitali muda mrefu.

Jackqueline ana taasisi ya Dkt. Ntuyabaliwe ambayo aliianzisha kwa ajili ya kumbukumbu ya baba yake ambaye alikuwa daktari wa kina mama katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kupitia Taasisi hiyo kazi yao ni kutengeneza maktaba na kugawa vitabu hapa nchini wameshafanya kwa shule za Dar es salaam, Morogoro na Dodoma.

Previous articleHABARI PICHA: ELIMU YA MATUMIZI YA TUMBAKU YAVUTIA WATU WENGI BANDA LA TMDA SABASABA
Next articleMAGAZETI YA LEO J.MOSI JULAI 10-2021

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here