Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Adam Fimbo (kushoto) akizungumza na Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa Umma wa TFDA Bi. Gaudensia Simwanza (kulia) alipokuwa kwenye Banda la Taasisi hiyo kwenye maonesho ya Biashara ya 45 ya Kimataifa (Sabasaba) yaliyofunguliwa rasmi Julai 5,2021 na Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango.
Na: Mwandishi wetu, DAR.
Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Nchini (TMDA) imesema kuwa imejipanga kikamilifu kwa kujielekeza katika kutoaji wa elimu kwa wananchi juu ya madhara yatokanayo na utumiaji wa Tumbaku.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi mkuu wa Mamlaka hiyo Adam Fimbo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kwenye maonesho ya 45 ya Biashara Kimataifa (Sabasaba) ambapo ameeleza mikakati iliyopo ya udhibiti wa matumizi ya tumbaku huku akitilia mkazo utoaji wa elimu kwa wananchi.
Ameeleza kuwa upo umuhimu wa kuwaelimisha wananchi juu ya madhara yatokanayo na utumiaji wa tumbaku na kwamba anaamini kwa kuanza na elimu kutasaidia kuwafanya watu wengi ususani vijana kuacha kabisa matumizi ya tumbaku au bidhaa zinazotengenezwa na tumbaku.
“Jukumu letu la kwanza ni kuhakikisha kundi la vijana walio na umri chini ya miaka 18 hawahamasishwi au kushawishiwa kuingia katika matumizi ya tumbaku pia kuona ni jinsi gani wale ambao hawavuti sigara hawajiingizi kwenye uvutaji na wale ambao tayari wanatumia waache kwa kuanza taratibu mwisho waache kabisa” Amesema.
Ameongeza kuwa zipo sababu za msingi zinazowafanya kuelimisha jamii kuacha matumizi ya tumbaku ambazo ni pamoja na kuhepuka kupata magonjwa kama shinikizo la Damu na mapafu kujaa maji huku akisisitiza juu ya umuhimu wa kuwepo sehemu maalu za kuvutia sigara hasa kwenye maeneo yenye mikusanyiko ya watu.