Home LOCAL SHINYANGA YAJADILI NAMNA BORA YA KUKABILIANA NA MAJANGA YA MOTO.

SHINYANGA YAJADILI NAMNA BORA YA KUKABILIANA NA MAJANGA YA MOTO.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Philemon Sengati akiongea na viongozi wa mkoa wa Shinyanga kuhusu kujiweka tayari kuzuia majanga ya moto mkoani kwake. (kulia) ni Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga Zuwena Omary Jiri.

Kaimu Kmanda wa Jeshi la Zimamoto Shinyanga Bw.Edward Lukuza akitoa mada kwa viongozi wa mkoa wa Shinyanga kuhusu kujiweka tayari kuzuia majanga ya moto.

Na: Anthony Ishengoma – SHINYANGA.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dk. Philemon Sengati  jana alikutana na viongozi wengine mkoani Shinyanga kujadili na kuweka mikakati ya pamoja kwa lengo la kujadili namna bora ya kukabiliana na majanga ya moto ambayo yameanza kujitokeza nakuleta athari mbalimbali  katika baadhi ya  mikoa hapa Nchini.

Katika hotuba yake kwa viongozi hao wa Mkoa Dkt. Sengati alisema mpaka sasa hakuna ambaye amebaini uhalisia wa sababu za kujitokeza kwa majanga ya moto katika Taasisi mbalimbali lakini hatua yake hiyo ni kujipanga mapema ili kujilinda dhidi ya majanga hayo yasitokee mkoani Shinyanga.

‘’Tunataka kujipanga mapema kuepusha majanga haya sitokee katika Mkoa wetu badala ya kusubiri yakishatokea tuanze kujipanga kutafuta namna ya kufanya ili kupunguza ukubwa wa tatizo binafsi nitajisikia vibaya sana kama jambo hili litajitokeza katika mkoa huu’’. Aliongeza Dkt. Sengati.

Aidha Dkt. Sengati aliongeza kuwa suala la kukabiliana na majanga ya moto linakuwa rahisi kulifanyia kazi lakini changamoto kubwa ni kutojua sababu hasa inayosabasabisha majanga hayo kujitokeza na kudokeza kuwa migogoro ni suala mojawapo la linalochangia tatizo hilo.

Pamoja na kuangazia tahadhari hiyo ya moto Dkt. Sengati pia alitumia fursa hiyo kuwataka wananchi mkoani Shinyanga kuendelea kufuata maelekezo ya Wizara ya Afya katika kupambana na majanga ya Corona na kudai kuwa ni kwa bahati mbaya sana wagonjwa wapya wameendelea kujitokeza.

Kamishna  wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga  George Kyando aliwataka viongozi wa Shule na Taasisi mbalimbali kuweka walinzi wenye ujuzi na makini tofauti na hali ilivyosasa kwa shule nyingi kuajili walinzi wazee na wamasai ambao hawana mbinu za ulinzi kukabiliana na uhalifu.

Mkuu huyo wa Jeshi la Polisi Mkoa aliongeza kuwa walinzi wanaotakiwa kuajiliwa na shule au Tasisi nyinginezo kuajili walinzi ambao wana mafunzo ya ulinzi kama vile mafunzo ya jeshi la polisi mgambo au wale waliostaafu katika Taasisi za usalama wenye ujuzi na maarifa ya kufanya kazi hiyo.

Kamishna Kyando alishauri shule mbalimbali kuiga mbinu inayotumika katika mafunzo ya kijeshi ambapo kila bweni wanatakiwa kubaki wanafunzi wawili kulinda tofauti na sasa ambapo wanafunzi wote huenda madarasani kwa ajili ya maandalizi ya masomo na kutoa fursa kwa wahalifu kuingia mabwenini na kuyachoma.

Naye Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto Mkoa wa Shinyanga Edward Lukuza alisema ni muhimu sana kwa wasimamizi wa miundombinu ya ujenzi kuhakikisha wanawasilisha ramani za ujenzi katika jeshi la Zimamoto ili ziweze kukaguliwa na kupewa ushauri wa namna bora ya kuainisha miundombinu ya kukabiliana na majanga ya moto kabla ya kuanza ujenzi.

Kamanda Lukuza aliongeza kuwa hata pale ambapo wamekuwa wakifanya ukaguzi na kubaini tatizo na kutoa ripoti ya nini cha kufanya mara nyingi ushauri wao umekuwa hauzingatiwi na kuwataka viongozi hususani maafisa elimu kuhakikisha wanayafanyia kazi na kutaka miundombinu ya umeme kukaguliwa kila baada ya miaka mitatu kuepuka moto unaosababishwa na itilafu ya umeme.

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Bi. Jasinta Mboneko aliangazia suala la kuwatumia vijana wa skauti kwa lengo la kufanya ukaguzi na kutoa mafunzo kwa vijana kwani vijana hao ni sehemu ya wanafunzi jambo linalowawezesha kupata taarifa muhimu kuhusu huarifu katika maeneo ya shule.

Aidha Bi. Mboneko aliwataka viongozi wa Shule pamoja na Maafisa Elimu kutopuuza vijana wa skauti na lakini pia akawataka viongozi hao katika Wilaya yake kufanyia kazi mara moja mapendekezo yote yaliyotolewa na Jeshi la Zimamoto yakiwemo yale ya jeshi la Polisi.

Tahadhari hii ya majanga ya moto inakuja kufuatia uwepo wa matukio ya majanga ya moto katika badhi ya shule nchini kwa mikoa ya Geita, Simiyu, Morogoro na janga la hivi karibuni katika Soko la Kariakoo jijini Dar es Salaam.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here