Home LOCAL MEYA KUMBILAMOTO APONGEZA ZAHANATI YA ISIMILLA KARIAKOO

MEYA KUMBILAMOTO APONGEZA ZAHANATI YA ISIMILLA KARIAKOO

Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Omary Kumbilamoto, akikata utepe wakati wa uzinduzi wa Zahanati ya Isimilla.Kariakoo na Narung’ombe Wilayani Ilala ( Kulia )Diwani wa Kata ya Mchikichini, Azim Khan. Picha na Heri Shaaban
Diwani wa Kata ya Mchikichini Azim Khan (katikati)akimtambulisha Meya wa halmashauri ya Jiji LA Dar es Salaam Omary Kumbilamoto kwa       Watendaji wa Mchikichini wakati wa kuzindua Zahanati ya ISIMILLA iliyopo Kata ya Mchikichini Mtaa wa Narung’ombe Kariakoo (PICHA NA HERI SHAABAN)

NA: HERI SHAABAN, ILALA

Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Omary Kumbilamoto ameipongeza Zahanati ya Isimilla kwa kutoa huduma bora katika Kata ya Mchikichini ambayo haina kituo cha umma.

Ametoa pongezi hizo wakati wa uzinduzi wa zahanati hiyo uliokwenda sambamba na zoezi la uchangiaji damu kwa ajili ya kusaidia wagonjwa mbalimbali wenye uhitaji.

“Niwapongeze kwa huduma nzuri mnazozitoa mmefanya kazi ambayo tulitakiwa tufanye sisi kama jiji kwa sababu Kata ya Mchikichini haina zahanati. Pia tunashukuru mmeisaidia serikali katika changamoto ya ajira,” amesema Kumbilamoto.

Aidha ameahidi kuwa watahakikisha kata hiyo inapata kituo cha umma ili kuwapunguzia adha wananchi ya kwenda kupata huduma katika maeneo ya mbali. 

Naye Diwani wa Kata ya Mchikichini, Azim Khan, amesema kata hiyo ina mitaa mitatu ya Ilala Kota, Msimbazi Bondeni na Misheni Kota na kuomba wajengewe zahanati au kituo cha afya kinachomilikiwa na serikali.

“Tunawashukuru Isimilla kwa kuwapa huduma wananchi wetu lakini bado kilio chetu ni kupata zahanati yetu, wananchi wetu wengi wanakosa huduma…kuna wananchi wana maisha duni hawana sehemu ya kukimbilia iliyo karibu,” amesema Khan.

Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Isimilla, Dk. Alison Mjema, amesema zahanati hiyo ilianzishwa mwaka 2019 ambapo imekuwa ikitoa elimu ya afya, upimaji magonjwa mbalimbali na tiba, huduma ya mama na mtoto na ushauri nasaha.

Aidha amesema zahanati hiyo imetoa ajira kwa Watanzania 18 katika kada mbalimbali za afya na malengo yao ni kuwa na kituo cha afya.

“Pamoja na mafanikio tuliyoyapata pia tunakabiliwa na changamoto kadhaa hasa uhaba wa eneo. Hivyo, tunaomba tusaidiwe kama kuna jengo la serikali hata kama ni kwa kulikarabati au kuchangia gharama kadhaa ili tuweze kupanua huduma zetu,” amesema Dk. Mjema.

Kwa mujibu wa Dk. Mjema, kwa mwezi zahanati hiyo inahudumia zaidi ya wagonjwa 1,000 ambao wanatoka Kata za Mchikichini, Kariakoo, Gerezani na maeneo mengine ya Jiji la Dar es Salaam.

Mwisho.

Previous articleWAZIRI LUKUVI- MASTER PLAN MKOA WA DAR ES SALAAM IMEKAMILIKA.
Next articleSHINYANGA YAJADILI NAMNA BORA YA KUKABILIANA NA MAJANGA YA MOTO.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here