Na. WAMJW-Dar es Salaam
Serikali imefanya maboresho ya miundombinu kwenye uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam kwa ajili ya upimaji wa Virusi vya Corona kwa wasafiri wanaoingia nchini.
Hayo yamesemwa leo na katibu Mkuu Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi wakati alipotembelea uwanja huo akiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi(Sekta ya Uchukuzi) Mhe.Gabriel Migire.
Makatibu Wakuu hao wakifika uwanja wa ndege kwa wa ajili ya kujionea maboresho yaliyofanywa kwenye uwanja huo ikiwemo zoezi la upimaji wa Corona kwa wageni wanaoingia nchini. Aidha walitumia muda huo kujionea na kutatua changamoto mbalimbali.
Prof. Makubi amesema kuwa zoezi hilo limeanza muda sasa hapa nchini na kulingana na wasafiri kuongezeka hivyo Serikali imeona ipo haja ya kuboresha miundombinu kila wakati ili kuendana na idadi ya ndege zinazoingia na kuepusha kero za huduma kwa wananchi.
“Suala hili la upimaji sio la sekta moja hivyo tumeona ni vyema kuja pamoja na Katibu Mkuu Mwenzangu na kujionea ili tuweze kuboresha kwa upande wote sote, sasa hivi maboresho makubwa yamefanyika ikiwemo upande wa kutoa majibu ambapo msafiri anapokuwa amelipia anaweza kupata majibu yake moja kwa moja kwenye email yake bila kuchelewa.
Suala la namba ya malipo’control number’ Prof. Makubi amesema kuwa hivi sasa namba za malipo ya upimaji msafiri anaweza kupata hata akiwa nje ya nchi na kulipia hukohuko hivyo kuondoa usumbufu kwa wasafiri,pia wale wanaounganisha ndege wameweza kuwatenganisha kwenye makundi mbalimbali hivyo wanahudumiwa haraka na hivyo kurahisisha zoezi la upimaji. Aidha utolewaji wa majibu sasa umekuwa wa muda mfupi na abiria anaweza kutumiwa kwa email , bila kuhitaji kuchapisha cheti.
Aidha, amesema wameweza kuongeza sehemu za upimaji pamoja na watumishi ili kuweza kurahisisha licha ya kuhitaji kuongeza watumishi hao wawe wengi zaidi.
Hata hivyo katibu Mkuu huyo aliwataka wananchi na wageni kujipanga kwa kufuata taratibu za kuachiana hatua moja Kati ya mtu na mtu ili kuweza kuhudumiwa kwa mpangilio na kutokukaa muda mrefu”foleni haiwezi kuepukika sehemu yeyote hivyo ni vyema watu wakajipanga na kuhudumiwa bila usumbufu wowote kwani tumeweka utaratibu wa mtu kutokukaa kwa muda mrefu”. Alisisitiza.
Prof. Makubi amesema upo umuhimu wa kipimo hicho cha haraka cha Corona kwa msafiri kwa sababu kuwa na cheti ‘negative’ ambacho anakuja nacho msafiri kwani mtu anaweza kupata maambukizi njiani au hakupima kama inavyotegemewa na hiyo inasaidia kuepuka maambukizi kwa wananchi wengine
Wakati huohuo Prof. Makubi amesema katika kuboresha usimamizi wa huduma za afya kwenye uwanja huo Wizara yake imefanya mabadiliko kwa kumuondoa Meneja Mkuu anayesimamia afya katika viwanja na mipakani pamoja na Meneja Mfawidhi wa uwaja wa ndege wa kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es salaam, anayehusika na masuala ya Afya.
Prof. Makubi amefafanua kuwa kwa sasa kuna changamoto katika “Verification” ya majibu inayoleta mrundikano wa abiria na ameelekeza kufikia Jumanne iwe imetatuliwa
Aidha, Prof. Makubi amesema hivi karibuni wataanza kuelekeza wasafiri wote wasajili taarifa zao kabla ya kusafiri hivyo alikumbusha ni vyema kutembelea tovuti ya Wizara ya afya au kuingia moja kwa moja kwenye mfumo wa ‘Afya Msafiri’.
Aidha,Katibu Mkuu-Afya ameelekeza kuongezwa kwa watumishi na vifaa ili kutoa huduma kama hiyo katika Terminal 2 na VIP kufikia Jumanne wiki ijayo.
Naye, Katibu Mkuu Wizara ya ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi) Mhe. Gabriel Migire amesema ziara hiyo wameweza kubaini changamoto za vifaa, wataalam na huduma za kibenki ambapo wataalum wa uwanja huo wamewathibitishia kuzishughulikia na kuzipatia ufumbuzi.
Mhe.Migire amesema kuanzia siku ya jumanne wataanza kufuatilia kuona kama changamoto zilizopo kwenye uwanja huo zimepata ufumbuzi ili kama kuna jambo la kufanya jitihada wao watalifanya kazi na kuagiza kuanza kupatia taarifa za vikao vya kila siku kutoka kwa wataalam hao.
Katibu Mkuu Wizara ya ujenzi Mhe Mingire ameahidi Wizara yake kuendelea kuwa karibu na Wizara ya Afya ili kutatua kwa pamoja changamoto zilizobaki katika viwanja na kuelekeza ifanyike tathimini tena kabla ya Jumanne ya kukabili ongezeko zaidi ya wasafiri/Watalii kwa siku za usoni.
Makatibu Wakuu hao wawili, wamewashukuru wafanyakazi wote wanaojituma katika viwanja na mipaka yote na Serikali iko pamoja nao katika kuboresha huduma hizo na kuwaelekeza waongeze usimamizi na uratibu wa pamoja ili kupunguza kero zaidi kutoka kwa wasafiri.