Home LOCAL RC GABRIEL AIPONGEZA TARURA KUANZA KUTUMIA MFUMO MPYA ULIOBORESHWA WA UKUSANYAJI WA...

RC GABRIEL AIPONGEZA TARURA KUANZA KUTUMIA MFUMO MPYA ULIOBORESHWA WA UKUSANYAJI WA MAPATO KWA NJIA YA KIELEKTRONIKI (TeRMIS)

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) wakati wa kuutambulisha mfumo mpya ulioboreshwa wa ukusanyaji wa mapato kwa njia ya kielektroniki ujulikanao kama (TeRMIS) unaosimamiwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) ambao umeanza kutumika mkoani Mwanza.

Afisa Tehama kutoka TARURA Bw. John Malasa akitoa mafunzo ya mfumo mpya ulioboreshwa wa ukusanyaji wa mapato kwa njia ya kielektroniki (TeRMIS) kwa wadau wa usafirishaji Mkoa wa Mwanza kwa lengo la kuwaelimisha namna mfumo utakavyofanya kazi wakati wa mafunzo yaliyofanyika katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa jijini Mwanza

Waandishi wa Habari wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel (hayupo pichani) wakati wa kuutambulisha mfumo mpya ulioboreshwa wa ukusanyaji wa mapato kwa njia ya kielektroniki (TeRMIS) unaosimamiwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwenye mkutano uliofanyika katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa jijini Mwanza.

Na: Bebi Kapenya, MWANZA.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel amepongeza Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kuanza kutumia mfumo mpya ulioboreshwa wa ukusanyaji wa mapato kwa njia ya Kielektroniki ujulikanao kama “TARURA e-Revenue  Management Information System” (TeRMIS) katika Mkoa wa Mwanza.

Ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari wakati wa kuutambulisha mfumo huo ambao umeanza kutumika rasmi mkoani Mwanza tarehe 20 Julai, 2021.

Mhandisi Robert Gabriel ameeleza kuwa lengo la mfumo huo ni kuboresha ufanisi wa ukusanyaji wa mapato ya Serikali yatakayosaidia maboresho na maendeleo ya miundombinu ya barabara kwani mfumo utampa fursa mtumiaji wa maegesho kulipia ushuru wa maegesho kwa saa, masaa, siku, wiki au mwezi, pia mfumo utatoza ushuru wa vyombo vya moto vilivyoegeshwa kwenye maeneo ya maegesho tu na si vinginevyo na pia mfumo utasaidia wateja kufanya maombi na kulipia huduma kwa njia ya mtandao bila kufika ofisi za TARURA.

“Nitumie fursa hii kuwapongeza TARURA kuanza kutumia mfumo huu kwani utaleta tija katika ukusanyaji mapato ya Serikali na utoaji wa huduma kwa wananchi kwasababu malipo yatapokelewa serikalini moja kwa moja na malipo yote yatafanyika kwa kutumia kumbukumbu namba ya malipo”, amesema Mhandisi Gabriel.

Pia, Mkuu wa Mkoa ameeleza kuwa mtumiaji wa chombo cha moto akiegesha chombo kwenye maegesho atapatiwa kumbukumbu namba ya malipo, ambapo atatumia kumbukumbu namba hiyo kufanya malipo kwa kutumia mtandao wowote wa simu ya mkononi, matawi ya Benki au kupitia kwa Mawakala.

Aidha, Mhandisi Gabriel amewataka TARURA kuhakikisha elimu ya matumizi ya mfumo inafika kikamilifu kwa wananchi ili wawe na uelewa wa pamoja lengo kikiwa ni kuepusha malalamiko mbalimbali kutoka kwa wananchi.

Pia, Mkuu wa Mkoa ametoa wito kwa wananchi kupokea mabadiliko hayo na kuanza kulipa wao wenyewe ushuru wa maegesho ili kuepuka adhabu na faini zisizo za lazima.

Kwa upande wake Afisa Tehama wa TARURA, Bw. Shadrack Mahenge amesema mfumo wa kielektroniki wa ukusanyaji mapato yaani “TARURA e-Revenue Management Information System” (TeRMIS) unaosimamiwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) umeanza kufanya kazi katika Mkoa wa Iringa, Singida, Dodoma na Mwanza na unatarajia kusambazwa nchi nzima.

 

Previous articleWAZIRI LUKUVI ACHARUKA BAGAMOYO AWAWEKA NDANI MATAPELI WATANO WA ARDHI KWA TUHUMA ZA UTAPELI
Next articleWIKI YA PASS TRUST KUANZA LEO JULAI 22 JIJINI DODOMA

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here