NA: EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
Waziri wa Viwanda na Biashara Prof.Kitila Mkumbo ameipongeza Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) kwa kushirikiana na TEMDO pamoja na CARMATEC kuhakikisha kiwanda inachokisimamia cha KMTC kinatengeneza tela ambalo litasaidia kubeba mazao na bidhaa kwa wakulima.
Akizungumza uzinduzi wa tela hilo katika Maonesho ya 45 ya Kimataifa ya Biashara katika viwanja vya Mwalimu Nyerere JijiniDar es Salaam, Prof.Mkumbo amesema tela hilo linauzwa kwa bei ya shilingi milioni 8.3 ambalo unaweza kulliweka vijijini na kuweza kuajiri vijana wengi waliopo mtaani na kuwaingizia kipato katika kipindi cha mavuno.
“Tela hili limetengenezwa hapa hapa Tanzania , ambapo kiwanda chetu cha KMTC kipo, hii inaonesha kwamba viwanda vyetu kwakweli vinaweza kutengeneza bidhaa za msingi na moja ya malengo yetu ni kukidhi mahitaji ya soko la ndani ili tuanze kutumia na kula bidhaa ambazo tunazalisha sisi wenyewe hapa”. Amesema Prof.Mkumbo.
Nae Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe.Exaud Kigahe amesema uzinduzi wa tela hilo utaenda kuongeza thamani ya uzalishaji hasa katika sekta ya kilimo ambapo moja wapo ya changamoto kubwa ni kwenye usafirishaji mazao na bidhaa mbalimbali.
” Bidhaa zinakuwa zinaharibika au kutokufika kwa urahisi katika maeneo husika kwasababu ya kukosa vifaa maalumu na vya bei rahisi kwaajili ya kusafirishia mazao hayo na bidhaa mbalimbali”. Amesema Mhe.Kigahe.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Taifa la maendeleo (NDC), Bi.Rhobi Sattima amesema kuwa tela hilo lenye uwezo wa kubeba tani tano limebuniwa kwa kuzingatia vigezo vyote vya ubora, ufanisi na usalama wakati linapokuwa linafanya kazi na kuthibitishwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS).
Amesema kuwa tela hilo limetokana na wazo bunifu la kuwa na chombo cha kusafirisha pembejeo na mazao ya kilimo ambalo litakokotwa na trekta linalounganishwa katika kiwanda cha matrekta kilichopo katika eneo la mitaa ya Viwanda TAMCO, Kibaha.
“Tela hili limesafiniwa kwa ushirikiano kati ya NDC,TEMDO na CARMATEC. NDC walitoa wazo bunifu, TEMDO walihusika katika usanifu na michoro na CARMATEC walihusika katika kufanya majaribio ya tela hili”. Amesema Bi.Sattima.
Amesema moja ya mchango wa tela hilo kwenye uchumi ni pamoja na mapinduzi kwenye sekta ya kilimokwani mkulima anaweza kuzalisha bila ya kuwa na changamoto ya usafirishaji wa mazao na pembejeo.Hii itasaidia kypatikana kwa urahisi malighafi za kilimo kwa ajili ya uongezaji thamani katika viwanda.