NA: HERI SHAABAN (ILALA)
NAIBU Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Saad Khimji, amewataka madiwani wa Halmashauri hiyo waige mfano wa Diwani wa Kipawa Aidan Kwezi kwa kuandaa mashindano mbalimbali katika Kata zao .
Naibu Meya Kimji aliyasema hayo Katika Ufunguzi wa Michezo Kipawa ya kombe la Diwani kugombea Ngombe wa Shilingi milioni 1 .
“Michezo ni ajira pia Michezo afya pia ujenga mahusiano nawaomba madiwani wote wa Wilaya ya Ilala muige juhudi za Diwani mwezenu wa Kipawa amefanya jambo kubwa kuunganisha jamii pamoja hii ni sehemu yako ya kuacha kumbukumbu katika maeneo wanayoongoza” alisema Kimji .
Aliwataka madiwani wa Wilaya ya Ilala kushirikiana pamoja katika sekta ya Michezo kwa ajili ya kuitangaza Wilaya hiyo na kukuza vipaji kwa vijana ili waweze kuunda timu ya Wilaya hadi ngazi ya mkoa
“Ni vema madiwani tukawa na jambo ambalo tutakuwa tunalifanya kila mwaka kwa ajili ya kuacha kumbukumbu katika maeneo tunayaongoza, suala la mpira si burudani tu au afya, michezo kwa ujumla ni ajira kwa vijana. Vijana wengi sana wamenufaika kupitia mpira wa miguu mfano Mbwana Samata ameanzia kwenye michezo kama hii,” alisema
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Kipawa, Aidan Kwezi, amesema kata hiyo ina vipaji vingi lakini katika miaka ya karibuni michezo ilikuwa imelala kwahiyo amejipanga kuiinua.
“Nilivyoingia kwenye nafasi hii mwaka 2020 moja ya malengo yangu ni kuhakikisha tunainua michezo na kuwakusanya vijana pamoja ili tuweze pia kushirikishana mambo mengine ya kuinuana kiuchumi,” amesema Kwezi.
Amesema mshindi wa kwanza katika mashindano hayo atapata ng’ombe mwenye thamani ya Sh milioni moja wakati mshindi wa pili atapata mbuzi na mpira na timu nane zitakazoingia kwenye hatua ya robo fainali zitapata jezi. Pia kutakuwa na zawadi za mfungaji bora, kipa bora na kikundi bora cha ushangiliaji.
Katika ufunguzi wa mashindano hayo uliofanyika viwanja vya Shule ya Msingi Majani ya Chai, timu ya FC Bontown iliibuka mshindi kwa kupata mabao 2 – 1 dhidi Falsafa FC.
Mashindano hayo yatahusisha timu 32 za mpira wa miguu na timu nane za mpira wa pete.
Mwisho.