Home LOCAL MIFUMO YA ELEKTRONIKI KUTUMIKA KUJAZA FOMU ZA UHIARI WA KUPATA HUDUMA ZA...

MIFUMO YA ELEKTRONIKI KUTUMIKA KUJAZA FOMU ZA UHIARI WA KUPATA HUDUMA ZA CHANJO DHIDI YA CORONA.

Na: WAMJW – DOM.

Mkurugenzi wa Kinga Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Leonard Subi amesema kuwa Serikali imejiapanga kuwa na mifumo miwili ya kujaza fomu ya uhiari wa kupata huduma ya Chanjo ya Corona ikiwemo kupitia njia ya Kielektroniki na njia ya karatasi.

Dkt. Subi amesema hilo wakati akiongea katika Taarifa ya Habari iliyorushwa na TBC (ARIDHIO) ikiwa ni mwendelezo wa kutoa elimu kwa wananchi juu ya mlipuko wa tatu wa ugonjwa wa Corona na umuhimu wa Chanjo ili kupambana dhidi ya ugonjwa huo. 

“Utaratibu ambao Serikali imeweza kuuweka ni kwamba, tutakuwa na mifumo ya aina mbili moja itakuwa ni mifumo ya kielektroniki ambapo mtu anaweza akatoa uhiari wake kwa kujaza mwenyewe kwamba anahitaji kwenda katika kituo Fulani kupata chanjo za ugonjwa wa COVID-19” Dkt. Subi.

Aliendelea kusema kuwa, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto  imekuwa ikiendelea kutoa Elimu kwa Wananchi juu ya huduma mbali mbali za tiba ana kinga, hivyo kusisitiza kuwa baada ya utoaji wa Elimu, mwananchi anakuwa na uhiari wa kupata huduma au kutopata. 

“Sisi kama Wizara ya afya tumekuwa tukiwapatia Wananchi elimu ya kutosha juu ya huduma fulani, sasa ukishampatia elimu ya kutosha , mwananchi anakuwa na uhiari wa kupata huduma au kutoipata, sawa sawa na mgonjwa anapoenda kufanyiwa huduma za upasuaji, tumekuwa tukimpatia huduma ya fomu ya uhiari” Dkt. Subi  

Aidha, Dkt. Subi amesema kuwa, hiari inaweza kuwa kwa njia ya mdomo au kwa njia ya maandishi, hivyo  katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Corona Serikali ikaona ni vizuri kwa Watanzania kuendelea kutoa hiari yao katika kupata huduma hizi za Chanjo ya Corona. 

Mbali na hayo Dkt. Subi aliwatoa hofu wananchi kwa kusema kuwa, Chanjo za ugonjwa wa Corona ni bora, salama, zina ufanisi wa kutosha na zimeorodheshwa na Shirika la Afya Duniani kwaajili ya matumizi ya dharura ili kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa wa Corona.

“Chanjo hizi ni salama na zina ufanisi wa kutosha lakini pia ni bora, tunaposema Chanjo hizi zimeweza kuorodheshwa na Shirika la Afya Duniani kwaajili ya matumizi ya dharura hususan katika kipindi hiki ambacho Dunia imekubwa na wimbi kubwa la ugonjwa wa COVID – 19” alisema Dkt. Subi 

Alisisitiza kuwa, Serikali imedhamiria kwa dhati kuutokomeza ugonjwa wa Corona, na ndio maana inatumia afua zote za kupambana dhidi ya maambukizi ikiwemo uvaaji sahihi wa Barakoa, kunawa mikono kwa sabuni na maji safi tiririka, kuepuka misongamano isiyo ya lazima, kutumia vipukusi, kufanya mazoezi na matumizi ya Chanjo ya ugonjwa wa Corona.

Hata hivyo, Dkt. Subi amewatoa hofu Watanzania na kuwataka waendelee kuiamini Serikali na kufuata maelekezo yote kutoka kwa Wataalamu wa Afya katika mapambano dhidi ya ugonjwa huu wa Corona, huku akisisitiza kuwa Sayansi haiwezi kupindishwa na maneno ya mitandao ya kijamii.

 MWISHO.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here