Home LOCAL LENGO LA SERIKALI KUHAKIKISHA TUNABORESHA MAWASILIANO KATIKA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI-DKT.NDUGULILE

LENGO LA SERIKALI KUHAKIKISHA TUNABORESHA MAWASILIANO KATIKA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI-DKT.NDUGULILE

Waziri wa Habari,Mawasiliano Sayansi na Teknolojia Dkt. Faustine Ndugulile akizungumza na waandishi wa habari leo katika ofisi za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) mara baada ya ujio wa Waziri wa Tehama na ubunifu kutoka nchi ya Rwanda Bi.Paula Ingabire.

Waziri wa Tehama na ubunifu kutoka nchi ya Rwanda Bi.Paula Ingabire akizungumza na waandishi wa habari leo katika ofisi za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).(PICHA ZOTE NA EMMANUEL MBATILO)

Na: Emmanuel Mbatilo DAR ES SALAAM.

Waziri wa Habari,Mawasiliano Sayansi na Teknolojia Dkt. Faustine Ndugulile amesema Serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali ili kuhakikisha mawasiliano yanafika katika maeneo yote ya nchi kwani mawasiliano ni haki ya msingi ya kila mwananchi.

Dkt. Faustine Ndugulile ameyasema hayo mara baada ya kumpokea Waziri wa Tehama na ubunifu kutoka nchi ya Rwanda, Paula Ingabire ambaye amefanya ziara nchini na kutembelea Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA )yenye lengo la kukuza mahusiano baina ya nchi hizo mbili.

Amesema mawasiliano ni kitu cha muhimu na Cha lazima na haki ya kila mtu ambapo serikali imewekeza zaidi katika mkongo wa taifa kama njia kuu ya mawasiliano Nchini.

“Lengo la Serikali ni kuhakikisha katika jumuiya ya Afrika Mashariki tunaboresha mawasiliano sisi kama Tanzania tunakuwa kitovu cha mawasiliano katika ukanda wa afrika Mashariki na kati.”amesema Dkt Ndugulile.

Amesema nchi ya Tanzania na Rwanda zimekuwa na mahusiano ya karibu yanayohusu tehama na mawasiliano ambapo katika mazungumzo yao wamekuwa kubaliana kuboresha mahusiano yaliolenga zaidi kubadilishana uzoefu.

” Nchi hizi mbili zinamahusiano ya muda mrefu ambapo tumeweza kupiga hatua kubwa sana katika sekta ya mawasiliano na tehama vilevile tumekuwa tukitegemeana katika masuala ya mawasiliano”amesema

Aliongeza kuwa Tanzania ni nchi ambayo imekuwa ikipeleka mawasiliano katika nchi 7 zinazoizunguka huku nchi mbili ndio zimebakia na kueleza kuwa kazi kubwa kwa sasa ambayo inafanyika ni kuunganisha Tanzania na Msumbiji.

Dkt Ndugulile amesema serikali imekuwa ikifanyika tathimini na upembuzi yakinifu katika kuhakikisha nchi ya DRC nayo inapelekewa mawasiliano.

Alibainisha kuwa lengo la mahusiano ya Nchi ya Tanzania na Rwanda ni kujenga mahusiano, kubadilishana uzoefu, kubadilishana utaalamu na wataalamu.

Hata hivyo Dkt Ndugulile amesema mkongo wa taifa ndio njia kuu ya mawasiliano ambapo serikali imejenga zaidi ya kilometa 7910 huku Ujenzi ukiendelea wa kilometa elfu 4490.

Pia amesema asilimia 94 ya watanzania wamefikiwa na mawasiliano huku katika maeneo ya kijografia yamefikiwa kwa asilimia 66.

“Kama Serikali tumewekeza kuhakikisha tunaporesha mawasiliano ambapo kwa kusambaza kwa kutumia mkongo wa taifa tunaimani gharama zitapugua za mawasiliano”amesema

Vilevile amesema serikali imefanikiwa kuhakikisha upatikanaji wa vifaa tehama ikiwa ni pamoja na simu janja zinakuwa na gharama ndogo.

“Serikali imefuta Kodi ili simu hivi sasa ziweze kushuka bei ili watanzania wengi waweze kuwa na uwezo wa kununua”

Amesema baadhi ya maeneo mengine serikali inaendelea kuyafanyia kazi ambapo jumla ya Billioni 45 zimetegwa kwa ajili ya maboresho ya mawasiliano pembezoni mwa nchi .

Kwa upande Waziri wa Tehama na ubunifu kutoka nchi ya Rwanda Bi.Paula Ingabire amesema Rwanda itaendelea kushirikiana na nchi ya Tanzania katika kuhakikisha inaboresha zaidi huduma za mawasiliano.

Amesema miongoni mwa makubaliano waliyokubaliana ni pamoja mabadiliko ya tehama na kidigitali baina ya nchi hizo zinafanya kazi kwa pamoja ili kuleta maendeleo ya tehama.

Previous articleMIFUMO YA ELEKTRONIKI KUTUMIKA KUJAZA FOMU ZA UHIARI WA KUPATA HUDUMA ZA CHANJO DHIDI YA CORONA.
Next articleMAGAZETI YA LEO J.MOSI JULAI 17-2021

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here