Home LOCAL “MARUFUKU KWA HOSPITALI ZA UMMA NA BINAFSI KULIPISHA WANANCHI GHARAMA ZA CHANJO”-...

“MARUFUKU KWA HOSPITALI ZA UMMA NA BINAFSI KULIPISHA WANANCHI GHARAMA ZA CHANJO”- SERIKALI

Na: Andrew Chale, DAR

SERIKALI kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imetoa angalizo kwa wasimamizi wa chanjo kutolipisha watu fedha kwani chanjo hizo ni bure huku ikihimidha kuzingatiwa kwa weledi.

Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu (Afya) , Prof. Abel Makubi wakati wa usambazaji  wa chanjo hizo kwenda mikoa mbalimbali nchini tukio lililofanyika bohari kuu ya dawa MSD, Kurasini Dar es salaam.

Akitoa rai kwa wasimamizi, Prof. Makubi alisema utoaji wa chanjo hizo kwenye hospitali za Umma na binafsi utatolewa bila kulipisha gharama za chanjo.

“Naelekeza kwa huu mgao wa Covax Facility ni marufuku Hospitali za umma au binafsi kulipisha Wananchi gharama yoyote katika zoezi hili la chanjo na lifanyike kwa uadilifu na kwa haki kwa walengwa wa sasa.” Alisema Prof. Makubi.

Ameongeza kuwa, Pamoja na Serikali ya awamu ya Sita chini ya Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, kufanikisha upatikanaji wa chanjo hizo na kuanza kuchanja Wananchi, Wizara ya afya inaendelea kuwashauri Wananchi kujikinga na UVIKO-19.

“Kwa kuzingatia kanuni za UVIKO 19, tunapaswa kunawa mikono, kuvaa barakoa, kukaa umbali za mita moja au zaidi, kuepuka misongamano na kufanya mazoezi.

Aidha, amesema ugawaji wa chanjo umezingatia taarifa ya visa vya wagonjwa waliohisiwa kuwa na UVIKO-19, idadi ya walengwa kwa kundi la kipaumbele pamoja na idadi ya chanjo zilizopatikana kwa sasa.

Katika hatua nyingune Serikali kupitia mamlaka ya dawa na vifaa tiba (TMDA), Maabara ya Mkemia Mkuu, Maabara kuu ya Taifa na Vyombo vingine vyote vimehakiki na kujiridhisha usalama na ubora wa chanjo za Janssen kutoka Kampuni ya Johnson & Johnson nchini Marekani. 

Prof. Makubi amebainisha kuwa, kutokana na Mwongozo wa Chanjo wa Taifa dhidi ya Ugonjwa wa UVIKO, Shirika la Afya Duniani (WHO), maelekezo ya Covax Facility na upungufu wa uzalishaji wa chanjo toka viwandani, Chanjo hizo kwa sasa zinatolewa kwa kufuata vipaumbele vya makundi yenye uhitaji mkubwa.

“Makundi ambayo yataanza chanjo ni pamoja na: Watumishi wa sekta ya Afya, Watu wazima umri wa miaka 50 na kuendelea na Watu wenye magonjwa. Kama ambavyo Serikali imekuwa ikieleza, uchanjaji kwa makundi yote nchini ni wa hiari au huru kwa kila mwananchi.

Kwa kuwa chanjo zilizopokelewa kwa sasa hazitoshelezi walengwa wa makundi yote nchini, makundi mengine yatapata chanjo katika awamu inayofuata, mara zitakapowasili.” Alisema Prof. Makubi.

Hadi sasa Serikali inategemea kutoa chanjo kwa makundi yanayolengwa kuanzia tarehe 3 Agosti 2021, siku ya Jumanne, katika vituo 550 vya kutolea huduma katika mikoa yote ya Tanzania bara ambapo Orodha ya vituo hivyo inapatikana pia katika tovuti ya wizara; www.moh.go.tz. 

Wananchi wote walengwa, wanaotaka kuchanjwa kwa hiari yao, huku wakitakiwa; Kujihakiki kama wapo ndani ya makundi matatu ya walengwa kwa sasa.

“Mlengwa atakayepata chanjo kuandaa kitambulisho cha Kazi, NIDA, Leseni ya Udereva, Mpiga kura, Pasi ya Kusafiria au kitambulisho chochote kinachotambulika kisheria.

Kufanya ‘booking’ ya siku ya kuchanjwa kwa kutumia mtandao ndani ya simu/Computer (online) yako kupitia https://chanjocovid.moh.go.tz au kwa kwenda moja kwa moja kwenye kituo na kujisajili kuanzia Jumatatu tarehe 2 Agosti 
2021.” Alisema Prof. Makubi.

Pia ameongeza kuwa, mlengwa atatakiwa kujaza fomu ya uhiari wa kuchanjwa, Ambapo Wizara inaagiza Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya nchini, kukamilisha 
matayarisho yote muhimu kwa utoaji wa chanjo, ili ifikapo tarehe 03 Agosti 2021, utoaji wa chanjo uwe umeanza katika vituo vilivyoainishwa katika mikoa.

Kutokana na uhitaji na mipangilio ya Mkoa husika, wanaweza kuongeza idadi ya vituo ili kupunguza msongamano katika vituo. Aidha, katika zoezi hili, wananchi, watasajiliwa katika mfumo wa Taifa wa Chanjo na watapatiwa cheti baada ya kuchanjwa.
 
“Mwisho, napenda kurudia tena kuishukuru Serikali yetu ya Mhe. Rais Samia Suluhu 
Hassan na Serikali ya Marekani, kwa kufanikisha upatikanaji wa chanjo hizi ambazo zimepitia kwenye mpango huo wa Covax. 

Pia nawashukuru wadau wetu wote wa chanjo kwa michango yenu mikubwa katika kufanikisha upatikanaji wa chanjo. Aidha 
Serikali inawapongeza sana Viongozi wetu na Wananchi ambao tayari wameitikia 
zoezi la kuchajwa kwa hiari” Alimalizia Prof. Makubi.

Mwisho.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here