Home LOCAL KITUO CHA KUPOZA UMEME KUJENGWA KONGWA.

KITUO CHA KUPOZA UMEME KUJENGWA KONGWA.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani(kulia) akizungumza na wakazi wa Kibaigwa wakati wa ziara yake ya kukagua miundombinu ya umeme katika Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma, Julai 27, 2021.


Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (katikati), Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Antony Mtaka (kushoto) na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mbunge wa Kongwa, Job Ndugai( kulia) akizungumza na wakazi wa Kijiji cha Machenje kitakapojengwa kituo cha kufua umeme cha Kongwa, wakati wa ziara ya Waziri wa Nishati ya kukagua miundombinu ya umeme katika wilaya hiyo, mkoani Dodoma, Julai 27, 2021.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (pili kushoto), Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Antony Mtaka (tatu kushoto ) na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mbunge wa Kongwa, Job Ndugai (nne kushoto) pamoja na viongozi wengine wakiwasili katika Kijiji cha Mbande, kutakapofungwa kifaa cha AVR wakati wa ziara ya kukagua miundombinu ya umeme katika wilaya ya Kongwa, mkoani Dodoma, Julai 27, 2021.

Na: Zuena Msuya, DODOMA.

Waziri wa Nishat, Dkt.Medard Kalemani amesema Serikali itajenga kituo kikubwa cha kupoza Umeme katika Wilaya ya Kongwa ili kumaliza tatizo la kukatika umeme mara kwa mara na kuboresha  upatikanaji wa Umeme katika wilaya hiyo na maeneo jirani.

Dkt. Kalemani alisema hayo wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua miundombinu ya umeme ikiwa ni pamoja na kutembelea eneo litakalojengwa kituo hicho lililopo katika Kijiji cha Machenje Kata ya Ugogoni Wilayani ya Kongwa mkoani Dodoma,Julai 27,2021.

Katika ziara hiyo, Dkt. Kalemani alisema kuwa tayari eneo la ukubwa wa Hekari 130 limepatikani ambalo litatumika kujenga kituo hicho, kitakachokuwa na uwezo wa kufua umeme wa Kilovolti 220.

Aidha alisema kuwa tayari zaidi ya shilingi milioni 63 zimetengwa kwa ajili ya kuwalipa fidia wakazi wa eneo hilo watakaopisha Ujenzi wa Mradi husika ambao utagharimu kiasi cha shilingi Bilioni 41.2.

Ujenzi wa kituo hicho unatajia kuanza kutekelezwa mapema mwezi Septemba mwaka huu 2021.

“Tuna umeme mwingi sana Mkoa wa Dodoma, lakini kuna changamoto kubwa kukatika umeme na wenye nguvu ndogo katika maeneo yote ya Wilaya ya Kongwa, kwa kipindi cha miaka mingi sana, hii inatokana na umeme huo kusafiri umbali mrefu kutoka kituo cha Zuzu hadi kufika huku takribani kilomita 120 na mzunguko ni takribani Kilomita 2000, suluhisho la kudumu ni ujenzi wa kituo cha kufua umeme ambacho kitamaliza kabisa tatizo hilo na kuwa historia, hasa katika Viwanda, Wafanyabiasha na watumiaji wengine”, alisema Dkt. Kalemani.

Hata hivo alisema kuwa, katika kutatua tatizo la kukatika Umeme mara kwa mara katika maeneo ya Mbande, Kibaigwa, Kongwa, Mpwapwa na Kiteto, ndani ya wiki hii kitafungwa kifaa maalum, kinachojulikana kama AVR ili kuuongeza nguvu ya Umeme katika maeneo hayo.

Dkt. Kalemani alifafanua kuwa kifaa hicho tayari kimeshatoka mkoani Ruvuma kuja Dodoma na kufungwa katika eneo la Mbande.

Sambamba na hilo kazi ya Ujenzi wa Njia ya kusafirisha Umeme wa kV 220 inaendelea kujengwa kutoka Zuzu kupitia Mpunguzi hadi kufika wilayani humo ili kupunguza tatizo la kukatika kwa Umeme mara kwa mara katika maeneo tajwa na mengine jirani.

Ujenzi wa njia hiyo ya umeme umefikia zaidi ya 55%.

Kufuatia utekelezaji wa miradi hiyo, aliwataka wakazi wa maeneo hayo kuvuta subira wakati tatizo la kukatika Umeme na kusambaza Umeme katika maeneo ambayo hayakufikiwa likitatuliwa hivi karibu.

Aidha aliweka wazi kuwa kuanzia mwaka wa fedha ujao, mkoa wa Dodoma utagawanywa Kitanesco na kuwa kama majiji mengine ikiwemo Dar es Salaam kwa lengo la kuimarisha na kuboresha huduma za umeme kwa wateja.

Vilevile alitumia ziara hiyo kukipandisha hadhi kituo cha umeme cha Kibaigwa kuwa kituo cha Wilaya ili kuimarisha na kuboresha upatikanaji wa umeme katika maeneo hayo.

Akizungumzia suala la usambazaji wa umeme vijijini, Dkt. Kalemani alimtaka mkandarasi kuongeza kasi katika kutekeleza kazi hiyo na kwamba wananchi wote waliolipia waunganishiwe umeme kwa wakati.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Antony Mtaka aliwataka wakazi wa eneo litakalolegwa kutuo cha kupoza umeme kuwa walinzi wa kituo hicho na kutoa ushirikiano kwa watakaotekeleza kazi hiyo.

Vilevile aliwataka wakazi wa maeneo ambayo bado hayajafikiwa na umeme kujiandaa kuupokea umeme huo kwa kutandaza nyaya katika nyumba zao pamoja na kulipia ili kuwa tayari kuunganishiwa umeme.

Mkoa wa Dodoma unawakandarasi 3 ambao watakaotekeleza mradi wa kusambaza umeme katika vijiji vyote vilivyosalia kwa kipindi cha miezi 12 na kwa gharama ya shilingi 27,000 tu.

Mkoa wa Dodoma kwa sasa unaongoza kwa kuwa na megawati zaidi ya 640 za umeme ukifatiwa na mkoa wa Dar es Salaam wenye megawati zaidi ya 500.

 

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here