Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) kimesema kuwa kimeanzisha shahada ya kwanza ya usimamizi wa rasilimali za nyuki ambapo Programu hiyo ikiwa ni ya kwanza kutolewa nchini inalenga kuzalisha watalaam waliobobea kwenye ufugaji nyuki, uzalishaji wa asali na mazao yatokanayo na nyuki.
Akizungumza nawaandishi wa habari kwenye maonesho ya 16 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia Jijini Dar es Salaam mhadhiri wa chuo hicho Dk Innocent Babili amesema kuwa amesema kuwa kozi hiyo inatolewa katika kampasi ya Katavi ambako pia wanafunzi wanapata fursa ya kujifunza kwa vitendo.
“Tumeipeleka hii program Katavi kwa kuwa kuna maeneo ya kufugia nyuki na wanafunzi wataweza kujifunza kwa vitendo. Mwitikio umekuwa mzuri, vijana wengi wameonekana kuichangamkia na kwa mwaka mpya wa masomo tunatarajia kudahili wanafunzi 100.
“Kozi hii tumeianzisha kwa kusudi maalum la kutengeneza wataalam ambao watasaidia kuongeza kiasi na ubora wa asali inayozalishwa nchini ili kukidhi viwango vya kimataifa. Kama nchi bado hatujatumia vizuri rasilimali za misitu na nyuki, miundombinu na uwezo tulionao ni mkubwa lakini tunazalisha kidogo yani chini ya uwezo wetu,” alisema Dk Babili
Sambamba na kuzalisha watalaam katika kampasi hiyo ya Katavi pia inatoa mafunzo ya muda mfupi kwa wakazi wa jirani na chuo hicho wanaojihusisha na ufugaji nyuki.
Kwa upande wake Afisa udahili wa chuo hicho Christopher Ndaga amesema kuwa kozi hiyo inahusisha ufugaji wa nyuki, jinsi ya kuwatunza na kuweza kuzalisha asali ya kutosha na mazao mengine yanayotokana na nyuki na kwamba kutaongeza tija kwa wafugaji nyuki na wazalishaji asali kwa ujumla na kuweza kukuza kipato na kuimalisha uchumi wao kwa ujumla.