Home LOCAL SERIKALI YAWATAKA WAFUGAJI KUJIUNGA KWENYE VYAMA VYA USHIRIKA

SERIKALI YAWATAKA WAFUGAJI KUJIUNGA KWENYE VYAMA VYA USHIRIKA

Mkurugenzi wa Utafiti, Mafunzo na Ugani kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Angelo Mwilawa akieleza kuhusu malisho ya nyasi zilizosindikwa au “Hey” kama yanavyojulikana kitaalam wakati timu ya wafugaji na wazalishaji wa malisho ya mifugo kutoka mikoa ya Njombe, Mbeya, Tanga na Kilimanjaro walipofika kwenye shamba la kikundi cha Mkaff kilichopo kijiji cha Ngarenairobi Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro leo (03.06.2021).

Na: Omary Mtamike, WIZARA YA MIFUGO, KILIMANJARO.
Serikali imewataka wafugaji kote nchini kujiunga na vyama vya ushirika ili waweze kutekeleza shughuli zao za ugani kwa tija.

Hayo yamesemwa leo (03.06.2021) mkoani Kilimanjaro na Mkurugenzi wa Utafiti, Mafunzo na Ugani Dkt. Angelo Mwilawa wakati akihitimisha ziara ya siku 7 ya wafugaji na wazalishaji wa vyakula vya mifugo kutoka mikoa ya Njombe, Mbeya, Tanga na Kilimanjaro.

Dkt. Mwilawa amebainisha kuwa kupitia ushirika wafugaji na wazalishaji wa malisho ya mifugo wataweza kupata huduma zao zote za msingi kwa urahisi ikiwa ni pamoja na pembejeo na zana mbalimbali ambazo wanaweza kuzitumia kwenye shughuli zao za ugani.

“Kwa mfano tumeona wilaya ya Hai kuna ushirika ambao umefanikiwa kununua mashine na kuweka kiwanda cha chakula bora cha mifugo jambo ambalo limewasaidia wafugaji waliopo kwenye ushirika huo kupata chakula cha mifugo yao na tumeona hata uzalishaji wa maziwa kwa wafugaji hao umeongezeka kwa asilimia 20 zaidi tofauti na ilivyokuwa hapo awali” Ameongeza Dkt. Mwilawa.

Dkt. Mwilawa ametoa rai kwa watanzania wenye nia ya kufanya biashara kuchangamkia  fursa ya biashara ya malisho ya mifugo kwa sababu mahitaji yake ni makubwa ikilinganishwa na kiwango kinachohitajika.

Kwa upande wake mmoja wa washiriki wa ziara hiyo kutoka mkoani Njombe, Rahel Mhema ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kuwawezesha kushuhudia kile kinachofanywa na wafugaji wenzao katika mikoa mingine ambapo ameomba kuongezeka  kwa ziara za aina hiyo ili waendelee kuongeza ujuzi zaidi katika kazi hiyo ya ufugaji.

“Nitoe wito na rai kwa vijana na wanawake wenzangu kuanza kufanya shughuli hii ya ufugaji kwa sababu una faida kubwa na unamfanya mfugaji kupiga hatua za maendeleo kadri siku zinavyoenda” Amesema Mhema.

Naye Kiongozi wa Shirika la kimataifa la utafiti wa malisho (CIAT), An Notenbaert amesema kuwa amefurahi kuona namna wafugaji na wazalishaji wa malisho walivyoweza kuboresha mifugo yao na kuongeza kiwango cha uzalishaji wa maziwa kupitia malisho yaliyoboreshwa ambapo amewasisitiza kuendelea kutunza mazingira wakati wote wa utekelezaji wa shughuli zao.

Mbali na wafugaji na wazalishaji wa malisho, ziara hiyo pia ilihusisha wataalam kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi na viongozi mbalimbali wa vyama vya ushirika vya wafugaji kutoka katika maeneo waliyotokea washiriki hao.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here