Home LOCAL RAIS SAMIA ASHIRIKI KIKAO CHA SADC MJINI MAPUTO, MSUMBIJI, AREJEA NCHINI, JIJINI...

RAIS SAMIA ASHIRIKI KIKAO CHA SADC MJINI MAPUTO, MSUMBIJI, AREJEA NCHINI, JIJINI DODOMA, LEO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akiwa katika Mkutano wa dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Joaquim Chissano mjini Maputo, Msumbiji leo. (Picha na Ikulu).


Maputo, Msumbiji, leo
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Samia Suluhu Hassan, ameshiriki Mkutano wa dharura wa Wakuu wa nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika mjini Maputo nchini Msumbiji, leo.

Taarifa iliyotolewa leo mjini Maputo, Msumbiji na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu Jaffar Haniu, imesema, Mkutano huo umejadili ajenda  mbalimbali zikiwemo zinazohusu mtangamano wa nchi wanachama wa jumuiya hiyo, fursa mbalimbali za kiuchumi, pamoja na changamoto za kiusalama.

Imesema, Mwenyekiti wa SADC ambaye pia ni Rais wa Msumbiji Filipe Jancinto Nyusi amesema jitihada za pamoja kutoka nchi wanachama wa ukanda wa SADC zinahitajika zaidi katika kukabiliana na tatizo la ugaidi linaloikabili nchi hiyo, kwani limekuwa likirudisha nyuma juhudi za maendeleo kwa Msumbiji na nchi wanachama.

Aidha, masuala mengine yaliyojadiliwa katika mkutano huo wa dharura ni  maambukizi ya Ugonjwa unaosababishwa na virusi vya Corona (UVIKO 19), uanzishwaji wa kituo cha majanga, masuala ya mabadiliko ya tabianchi, usalama wa chakula, biashara na Uwekezaji katika ukanda wa Jumuiya hiyo ya SADC.

Rais Nyusi amezisisitiza nchi wanachama kuendelea kuunga mkono jitihada za Taasisi za Utafiti  katika kufuatilia taarifa za kusambaa kwa UVIKO 19 na mawimbi mapya ya ugonjwa huo na kuendelea kuchukua tahadhari ili kuzuia maambukizi mapya.

Kuhusu changamoto za tabianchi, Rais Nyusi amesema baadhi ya nchi wanachama zimekumbwa na uhaba wa mvua na nyingine kupata mvua nyingi zaidi na kufanya uwepo wa uwezekano kwa baadhi ya nchi kukumbwa na uhaba wa chakula.

Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maenendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), umefanyika pamoja na Maadhimisho ya miaka 40 tangu kuanzishwa kwa Jumuiya hiyo, ikiwa na kauli mbiu “ Kuimarisha Amani na Usalama, Kuhamasisha Maendeleo na Ustahamilivu wa Changamoto Zinazoikabili Dunia”.

Rais Samia amemaliza ziara ya kikazi ya siku mbili nchini Msumbiji na kurejea Jijini Dodoma

Previous articleLENGO LA JUMUIYA YA KIISLAM YA AHMADIYYA NI KUWAFANYA WATU WAISHI KATIKA NJIA YA KUMPENDEZA MUNGU NA SIO SIASA AMA UGAIDI
Next articleTBS KUWASOGEZEA HUDUMA WADAU WA VIWANGO KWENYE MAONESHO YA SABASABA

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here