Home BUSINESS PSSSF NA BENKI YA AZANIA ZAZINDUA HUDUMA YA KUWAWEZESHA WANANCHI KUMILIKI NYUMBA...

PSSSF NA BENKI YA AZANIA ZAZINDUA HUDUMA YA KUWAWEZESHA WANANCHI KUMILIKI NYUMBA NA VIWANJA KWA GHARAMA NAFUU

Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, CPA. Hosea Kashimba(kulia) na Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya Azania Bw. Charles Itembe wakisaini makubaliano ya kuwawezesha wananchi kumiliki nyumba na viwanja kwa gharama nafuu.
Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, CPA. Hosea Kashimba(kulia) na Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya Azania Bw. Charles Itembe wakionyesha mikataba hiyo baada ya kusaini

Mkurugenzi wa Uwekezaji mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma, Bw. Fortunatus Magambo 

 

Baadhi ya wakurugenzi wa PSSSF na benki ya Azania walioshuhudia uzinduzi huo.

Mkurugenzi wa Uwekezaji mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma, Bw. Fortunatus Magambo (aliyesimama) akitoa neno la utangulizi. Wengine kutoka kulia ni CPA. Kashimba, Bw. Itembe na Meneja Mwandamizi wa Wateja  Binafsi Bw. Jackson Lolai 
Picha ya pamoja

NA: KHALFAN SAID

MFUKO wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) na Benki ya Azania, wamezindua huduma ya kuwawezesha wanachama wa Mfuko huo na wananchi kwa ujumla kuweza kumiliki nyumba kwa kulipa kidogokidogo.

Uzinduzi huo umefanyika jijini Dar es Salaam Juni 21, 2021 ambapo taasisi hizo mbili kupitia Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, CPA. Hosea Kashimba na Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya Azania Bw. Charles Itembe walisaini makubaliano yatakayowawezesha wananchama na wananchi kukopa kutoka benki hiyo kupitia mikopo ya makazi yaani (Mortgage loan) ili kununua nyumba na viwanja vinavyomilikiwa na PSSSF  kupitia uwekezaji iliyoweka sehemu mbalimbali nchini.

CPA. Kashimba alisema mradi wa nyumba za gharama nafuu upo Dar es Salaam, Morogoro, Shinyanga, Tabora, Mtwara na Iringa na mradi wa viwanja vya gharama nafuu viko katika mikoa ya Ruvuma, Kagera, Tabora, Iringa, Katavi, Morogoro, Dar es Salaam, Rukwa, Lindi na Mtwara.

“Kupitia makubaliano haya, wanachama wa Mfuko pamoja na wananachi wengine watafaidika kwa kukopeshwa nyumba na viwanja kwa riba ndogo ya asilimia 10% kwa mwaka na hivyo kuimarisha na kuweka mazingira wezeshi kwa wananchi kwenye maeneo hayo ili wawe na makazi bora na kutimiza kauli mbiu ya serikali ya nyumba bora kwa wananchi wote inawezekana.” Alibainisha CPA, Kashimba.

Akifafanua zaidi kuhusu masharti ya kukopa nyumba na viwanja Mkurugenzi Mkuu huyo alisema, mteja atalazimika kuweka rehani ya asilimia 10% ya thamani ya mkopo au mali ya thamani hiyo kwa dhamana ya mkopo na kiwango cha juu kabisa ambacho mteja anaweza kukopwa na benki ni asilimia 90% ya thamani yote ya nhyumba au kiwanja.

“Mteja atakapokamilisha malipo yake atakabidhiwa hati yake ya nyumba au kiwanja na benki ya Azania na muda wa marejesho ya mkopo ni kipindi kisichozidi miaka 15 kwa mkopo wa nyumba na miaka miwili kwa mkopo wa kiwanja.” Alifafanua CPA. Kashimba.

Alisema katika makubaliano hayo jumla ya nyumba 192 na viwanja 886 vyenye hati vitakuwa sokoni na vitauzwa kwa mkopo wenye riba nafuu kwa wanachama na wananchi  kwa kuzingatia vigezo na masharti mepesi yaliyowekwa na waitaji watapata fursa ya kutembelea na kuona viwanja hivyo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya Azania, Bw. Charles Itembe,
ameupongeza Mfuko wa PSSSF kwa kubuni mradi huo mkubwa wenye tija kubwa kwa taifa kwa Wanachama na wasio wananchama wa PSSSF.

“Kama Mfuko wa Hifadhi ya Jamii umeonyesha nia njema inayolenga kumuinua mwananchi kwa vitendo na sio kwa maneno tu.” Alisema.

Alisema Benki ya Azania inaona faraja kuwa sehemu ya mradi kwani ina uzoefu wa miaka mingi wa ukopeshaji wa nyumba Tanzania.

“Benki imeanza kutoa mikopo hiyo toka mwaka 2005 wakati huo mabenki mengine yalikuwa bado hayajaanza kufanya kazi hiyo.” Alisema.

Alisema ushirikiano huo benki na PSSSF sio jambo la kwenda kuiga kwani ni jambo ambalo wameshawahi kulifanya na kutoa manufaa makubwa kwa watu wengi na kujenga heshima kubwa sana huko mtaani.

“Napenda niwahakikishgie watanzania wanaokuja kuomba mikopo ya nyumba au viwanja, tuko tayari kuwahudumia na mikopo hii inatolewa kwa asilimia 10%, hakika ni riba ambayo ni ndogo sana.” Aliwahakikishia wahitaji.

Akifafanua zaidi alisema mtu atakayekopa atakuwa na muda mrefu wa kutosha kulipa kidogokidogo na anaweza kuwa tayari anakaa kwenye nyumba yake huku akiendelea kulipia.

“Mkopo huu utakuwa na bima ya mkopo kupitia huduma ya bank assurance inayotolewa na benki ya Azania, kwa hivyo nyumba yako itakuwa salama kwa majanga mbalimbali yanayoweza kusababishwa na moto au mafuriko.” Alisema Bw. Itembe.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here