Home LOCAL MAGANGA MKUU WA SERIKALI AFANYA ZIARA HOSPITALI YA AMANA.

MAGANGA MKUU WA SERIKALI AFANYA ZIARA HOSPITALI YA AMANA.

Na.WAMJW, Dsm.

Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Aifelo Sichalwe amefanya ziara fupi katika hospitali ya rufaa ya Mkoa Amana Jijini Dar es Salaam yenye lengo la kukagua Utekelezaji wa maagizo ya Viongozi wa Wizara waliyoyatoa kwa nyakati tofauti kuhusu maandalizi na utayari wa Watumishi wa afya katika kukabiliana na magonjwa ya mlipuko ikiwemo ugonjwa wa covid 19.

Akiwa hospitalini hapo Dkt. Sichalwe amezungumza na uongozi wa hospitali hiyo ambapo amewataka viongozi hao wa wafanyakazi kujitayarisha kwa vifaa na matibabu kwa ajili ya kukabiliana na magonjwa ya mlipuko.

Amesema Kama watumishi wa Afya, ni vyema kuwa tayari wakati wowote hususan katika kipindi hiki ambacho nchi jirani wamekumbwa na wimbi la tatu la ugonjwa wa Corona kwa kuwa raia wa nchi hizi wana muingiliano mkubwa wa shughuli za kiuchumi na biashara, hivyo kama nchi hatuna budi kujipanga.

Sambamba na kikao hicho Dkt.Sichalwe amekagua miundombinu ya hospitali na utekelezaji wa afua za kuzuia maambukizi mahali pa kazi (Infection, prevention and control). Ameupongeza uongozi wa hospitali hiyo kwa juhudi na jitihada kubwa wanayofanya hospitalini hapo kwa lengo la kuzuia ueneaji wa maambukizi kwani watumishi wote walikutwa wamevaa barakoa na sehemu za kunawia zenye sabuni na maji  zikiwepo kila wodi, sehemu ya mapumziko na getini. 

“Nimeona mmevaa barakoa, mnatoa elimu kwa wananchi pia. Haya mnayotekeleza hapa ni kama darasa kwa wananchi wote wanaokuja kupata huduma hapa nao watakuwa mabalozi kwa wenzao kwenye jamii. Nina imani utekelezaji huu mnaendeleza hata baada ya kazi”.

Aidha, Dkt.Sichalwe amewaagiza Waganga Wakuu wa Mikoa nchini kusimamia utekelezaji wa afua hii, kwani unatukinga siyo tu na ugonjwa wa covid 19 bali na Magonjwa mengine mengi yanayosababishwa na kula vitu kwa mikono isiyo safi na kuvuta hewa yenye vimelea vya maambukizi.

Vilevile Dkt.Sichalwe ametembelea mtambo maalumu wa kuzalisha hewa ya Oksijeni hospitalini hapo ambapo ameipongeza Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwekeza zaidi ya Milioni 600 ili kuhakikisha wanaokoa Maisha ya watanzania wanaohitaji huduma hiyo.Mtambo huo wenye matoleo Zaidi ya 89, unauwezo wa kuzalisha mitungi 200 ya hewa ya Oksjeni kwa masaa 24 na hospitali ina uwezo wa kuhudumia watonjwa wenye uhitaji 150 kwa wakati mmoja.

Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Dkt. Rashid Mfaume amesema kuwa juhudi hizo zinaendelea kufanywa na hospitali zote ndani ya Dar es Salaam ili kuhakikisha wanalidhibiti ipasavyo wimbi hili la tatu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here