Home LOCAL LHRC YALAANI TUKIO LA KUCHOMWA MOTO MTOTO WA KIKE WA MIAKA MINNE.

LHRC YALAANI TUKIO LA KUCHOMWA MOTO MTOTO WA KIKE WA MIAKA MINNE.

DAR ES SALAAM.

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimelaani tukio la kuchoma moto nyumba ambayo ndani yake kulikuwa na mtoto wa kike mwenye umri wa miaka minne (4) ajulikanae kwa jina la Nyanzobhe Mwandu.

Tukio hilo limetokea Juni 16, 2021 katika Kijiji cha Kombe, Kitongoji cha Songambele, Kata ya Usinge, Mkoa wa Tabora ambapo inadaiwa kuwa watu waliotekeleza ukatili huo ni Askari wa Mamlaka ya Usimamizi wa Hifadhi ya Wanyamapori Tanzania (TAWA) wakishirikiana na Askari Polisi wa Kituo cha Polisi cha Igagala Namba 5 kwa amri ya aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kaliua.

Akizungumza na waandishi wa habari Juni 21, 2021 Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Anna Henga amesema Ibara ya 24(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 (kama ilivyofanyiwa marekebisho mara kwa mara) inasema kwamba, Kila mtu anayo haki ya kumiliki mali, na haki ya hifadhi ya mali yake aliyonayo kwa mujibu wa sheria.

Ameongeza kuwa, Ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 pamoja na marekebisho yake inatamka wazi kwamba, kila mtu anayo haki ya kuishi na kupata kwa jamii hifadhi ya maisha yake, kwa mujibu wa sheria. 

Kwa maana hiyo Mkuu wa Wilaya ya Kaliua amekiuka masharti ya Katiba ya nchi kwa kuagiza kuangamizwa kwa nyumba na mazao ya wananchi. Kitendo kilichofanywa na Mkuu wa Wilaya ya Kaliua kimepelekea kukatiza uhai wa mtoto Nyanzobhe Mwandu. Huu ni ukiukwaji wa Katiba ya nchi na pia ukiukwaji wa haki za binadamu.

“Kituo tunatambua na kupongeza hatua zilizochukuliwa na serikali dhidi ya aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kaliua na tunatarajia kuwa atawajibishwa kutokana na kitendo cha kukatisha maisha ya mtoto Nyanzobe Mwandu kilichosababishwa na amri yake kwa Askari wa TAWA na askari Polisi wa Kituo cha Polisi cha Igagala Namba 5,” amesema Henga.

Aidha Kituo hicho kimepongeza hatua zilizochukuliwa na serikali dhidi ya aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kaliua na kwamba wanatarajia kuwa atawajibishwa kutokana na kitendo cha kukatisha maisha ya mtoto huyo.

Credit – Diramakini Blog.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here