Home LOCAL KUTOKA BUNGENI JIJINI DODOMA MCHANGO WA MHE, DEO MWANYIKA MBUNGE WA JIMBO...

KUTOKA BUNGENI JIJINI DODOMA MCHANGO WA MHE, DEO MWANYIKA MBUNGE WA JIMBO LA NJOMBE MJINI

Na: Maiko Luoga

“Mhe, Naibu Spika nashukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia Bajeti hii ambayo ni bajeti ya kwanza katika Serikali hii ya awamu ya sita lakini bajeti ya kwanza katika mpango wa miaka mitano wa 2021/2022 kwenda mpaka 2025/2026”

“Dhima yake Mhe, Naibu spika ni uchumi wa Viwanda shindani na shirikishi, jambo hili linanigusa sana na nimelizungumzia sana hapa Bungeni, lakini kwanza nianze kumpongeza Mhe, Waziri na timu yake kwa kutupa Bajeti hii ambayo kwakweli imegusa mioyo ya Watanzania”

“Sisi Wabunge ni mashahidi mengi yaliyosemwa katika bajeti hii ni yale ambayo sisi kama Wabunge tuliomba Serikali iyashughulikie kwahiyo tunamshukuru sana Mhe, Rais Samia Suluhu Hassan kwakuwa chachu kubwa ya bajeti hii”

“Binafsi namshukuru Mhe, Rais kwanza ndani ya bajeti hii tunaona dhamira ya dhati ya kushirikisha sekta binafsi katika kuendesha uchumi wa nchi, Sekta binafsi ndio sekta ambayo tunaitegemea kupata mapato makubwa ya nchi”

“Mhe, Naibu Spika ndani ya bajeti hii tunaona wazi kabisa Mhe, Rais anatoa maono ya wazi na miongozo ya kuonesha kwamba miradi mbalimbali iliyokuwa ya sekta binafsi ambayo imekwama sasa ipate ufumbuzi na iweze kuendelea mbele”

“Kwa ufupi kabisa nimpongeze Mhe, Rais kwakutoa mwongozo kuhusiana na Mradi wa Mchuchuma na Liganga mradi huu mhe, Naibu Spika umezungumzwa kwa muda mrefu sana na ulifikia mahali ukawa kama ni wimbo unaoimbwa na kuisha”

“Sasa tunaona dhamira ya dhati kabisa ya Mhe, Rais kwamba majadiliano yale yaliyokuwa yamekwama yaweze kuendelea na kukamilishwa na kama hayawezekani basi tutafute namna nyingine, namshukuru sana Mhe, Rais kwa maamuzi hayo”

“Wote tunafahamu sekta ya kilimo inatoa mchango mkubwa sana kwenye uchumi wa nchi asilimia ishirini na sita ya pato ghafi la Taifa inatokana na sekta ya kilimo na asilimia sitini na tano ya Watanzania wa Vijijini wamejiajiri katika sekta hii ya kilimo”

“Mchango wa sekta hii kwa upande wa kuleta fedha ya kigeni ni takribani asilimia ishirini na nne, inashangaza kwamba sekta hii inatia huruma kwa maana pamoja na hizi namba tunazoziona hapa uwekezaji kwenye sekta hii bado ni mdogo sana na wengi wamelizungumza hili”

“Tunazungumzia asilimia sifuri nukta nane hadi tisa lakini ukweli ni kwamba asilimia za uwekezaji ni ndogo mno na sio kwa Serikali pekee kupitia bajeti lakini hata kwa Sekta binafsi, Mhe, Naibu Spika Benki zetu bado hazijachangamkia fursa kubwa ambazo zipo katika sekta hii kubwa ya kilimo”

“Ukiangalia mgawanyo wa fedha ambazo zimeenda kwenye sekta binafsi kwaajili ya kilimo inasikitisha kuona kwamba takribani asilimia thelathini na tano nukta nane ya mikopo ya benki inaenda kwenye mambo ya watu binafsi, asilimia kumi na tano nukta saba imeenda kwenye biashara za kawaida”

“Asilimia kumi zimeenda kwenye Viwanda lakini kilimo ni asilimia nane tu kwahiyo tuna tatizo kubwa la uwekezaji kwenye sekta hii upande wa Serikali kupitia bajeti lakini vilevile kupitia sekta binafsi”

“Mhe, Naibu Spika nadhani wote tuna kazi ya kufanya hapa lakini la kwanza kabisa tuanze na maamuzi ya kibajeti, naelewa hakuna kitu ambacho tunaweza kufanya kwenye bajeti hii kwa sasa lakini tunaomba sana Serikali”

“Mhe, Waziri wote tutambue kwamba lazima tuitendee haki Tanzania na huwezi kuitendea haki Tanzania kama hautatoa fedha za kutosha kwenye sekta hii ya kilimo, katika miaka minne iliyopita sekta hii uwekezaji wake umeshuka lakini huko nyuma angalau tulifikia asilimia tano”

“Lakini tukiweza angalau kufika asilimia sita Mhe, Naibu Spika nadhani tutakuwa tunaenda katika mlolongo mzuri, hapa nitoe ushauri tunahitaji kuvutia wawekezaji kwa namna ya pekee kwenye sekta hii ya kilimo ninavyoona tunahitaji kuwa na skimu maalumu za sekta ya kilimo”

“Tunajua sekta hii hasa ipo katika maeneo ya Vijijini na Mikoani wengine walisema na mimi nasisitiza kuna haja ya kuwa na vivutio vya kikodi na kisera ambavyo vitajikita kwenye sekta ya kilimo na kwenye Viwanda ambavyo vitakua na kujengwa katika maeneo ya kilimo”

“Jambo tunaloliona sasa Kiwanda kinachojengwa katika eneo la kilimo Mikoani na kinachojengwa kwenye mikoa ambayo haina kilimo vinakuwa sawa hatuwezi kufika kwa utaratibu huo”

“Lakini Mhe, Naibu Spika Serikali imejitahidi kuweka vivutio vya aina Fulani katika bajeti hii lakini mimi nasema Mhe, Naibu spika kwamba pamoja na hilo tunawashukuru lakini bado tunatakiwa kuangalia wapi hasa panahitaji kuwekewa hivyo vivutio”

“Tuangalie mnyororo wa thamani katika sekta ya kilimo na mimi nasema Vifungashio sawa codrooms sawa lakini twende tukaangalie pale ambapo kunafanyika uzalishaji wa mazao yetu ya kilimo ndipo hasa tuweke hivyo vivutio”

“Tuangalie maeneo ambayo kama kuna Viwanda vya madawa, Mbolea na tuangalie vilevile pale ambapo tunahitaji utaalamu na hatuwezi kuupata hapo basi tulegeze masharti mbalimbali kwa watu ambao wataenda kufanya kazi kama Wataalamu kwenye sekta ya kilimo”

“Tunahitaji kufanya kazi kimkakati ili tuweze kuikomboa hii sekta ya kilimo, Mhe, Naibu Spika nizungumzie zao la Parachichi kwa kifupi, Nchi hii inauwezo mkubwa wa kuongeza mapato makubwa sana kama tukiweza kuwekeza kwenye zao la Parachcichi”

“Mhe, Naibu Spika zao hili linaweza kuibadili Tanzania ukichukua nchi kama Mexco ambayo eneo lake ni dogo hata ukubwa wa mkoa wa Njombe Mexco ni ndogo lakini kwa mwaka 2018/2019 kwa zao la Parachichi pekee Mexco wameingiza dola bilioni mbili nukta saba”

“Haya ni mapato yanayofikia mapato yetu yote ya dhahabu kwahiyo ipo haja ya kuliangalia hili jambo kwa umakini sana, lakini ukiangalia kwa sasa watafiti wanasema katika miaka mitano ijayo Tanzania inaweza ikawa nchi ya uzalishaji mkubwa wa Parachichi kuliko hata Kenya”

“Lakini tunaambiwa hapa kwamba Parachichi zetu sisi tunazisajili kama zinatoka Kenya kwa hiyo kuna upotevu wa mapato na nchi yetu inakosa fedha za kigeni, naomba niseme kwamba tatizo hili litaendelea kama tusipoweka mikakati mahili mapema ya kutatua hili”

”Ukiangalia kwenye Bandari yetu ya Dar Es Laam ambayo ndio kubwa tunayoitegemea, nchi hii inakadiliwa kuzalisha karibu tani lakisita za Parachichi pale ukienda ukalinganisha na Mombasa utaona utofauti”

“Watu wanaenda Mombasa kwasababu slot za Coadrooms zipo 1800 unaenda kwenye kontena una slot unasubiri meli, Tanzania Tiks pamoja na TPA Slot zipo 120 kwahiyo hakuna uwezo wowote utakaotufanya sisi tuende kwenye huo ushindani”

“Mhe, Naibu Spika nimalizie kwa kuzungumzia kidogo sekta ya Madini ukiangalia utakuta kwamba tumelegalega na kwa kiasi kikubwa nchi yetu sekta ya utalii imeshuka lakini sekta hii ya madini imebalansi na imenyanyua uchumi wa Taifa”

“Tunamshukuru Mungu kwamba tuna dhahabu lakini kwa kiasi kikubwa dhahabu yote hiyo imetoka kwenye migodi kama miwili pamoja na wachimbaji wadogowadogo, Mhe, Naibu spika mimi nasema kwamba tunatakiwa tuendelee kuvuta wawekezaji kwenye sekta hii ya madini ili tuweze kupata mapato makubwa zaidi”

“Lakini tunatakiwa tuende kwenye sekta nyingine ambazo sasa hivi ndiko Dunia inaenda na huko tuna wawekezaji kuna maeneo kama ya gesi tayari tuna wawekezaji lakini bado wanagombea mitaji na nchi nyingine”

“Kama hatutafanya maamuzi ya haraka inamaana hiyo nafasi haitakuwepo na hatutaweza kupata mapato makubwa ambayo kama tungekuwa na migodi kila mahali inafanya kazi na kuzalisha tungekuwa na uchumi mkubwa” alimaliza Mhe, Deo Mwanyika.

Previous articleNATAKA MJI WA KAHAMA UWE MJI WA KISTAREHE – DC KISWAGA
Next articleSERIKALI YAJIPANGA KUKOMESHA UKATILI WA KIJINSIA NDANI NA NJE. YA VYOMBO VYA HABARI

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here