Home LOCAL HATUTARUHUSU MTENDAJI ABAKI NA FEDHA AKISUBIRI MUDA WA NYONGEZA – WAZIRI MKUU

HATUTARUHUSU MTENDAJI ABAKI NA FEDHA AKISUBIRI MUDA WA NYONGEZA – WAZIRI MKUU

DODOMA.

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali haitaruhusu mtendaji wake abaki na fedha kwa uzembe halafu ategemee kupewa muda wa nyongeza baada ya mwaka wa fedha kuisha.

“Tunatarajia kufanya maboresho ya kanuni ambayo yataruhusu matumizi ya fedha miezi kadhaa baada ya mwaka fedha kuisha ili ziweze kukamilisha miradi ambayo haijakamilika. Hatutahitaji kuona mzembe akibaki na fedha bila kuzitumia, huku akitarajia kuwa atapewa muda wa nyongeza… wananchi wanahitaji kuona miradi ikikamilika.”

“Pamoja na maboresho hayo hatutamvumilia yeyote atakayekaa na fedha bila kuzitumia akitegemea kuongezewa muda. Tutaweka kipengele ambacho kitambana mtendaji wetu kuhakikisha kila fedha inayoingia inatumika kwa kipindi kinachotakiwa,” amesisitiza.

Ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Juni 3, 2020) Bungeni jijini Dodoma kwenye kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu wakati akijibu swali la Mbunge wa Singida Magharibi, Mheshimiwa Elibariki Kingu ambaye aliitaka Serikali ione umuhimu wa kubadilisha utaratibu wa kurejesha fedha zilizobakia kwenye Halmashauri kila inapofika Juni ambayo mwisho wa mwaka wa fedha.

“Serikali inapopeleka fedha kwenye Halmashauri kati ya Machi na Juni zisipotumika zote, fedha zinazobaki huwa zinarudishwa Hazina. Lakini fedha hizi huwa zimepangiwa miradi ya ujenzi wa mabweni au vituo vya afya na zikirudi zinachelewesha kukamilika kwa miradi husika. Je serikali haioni umuhimu wa kubadilisha utaratibu huu ili fedha hizo zitumike kukamilisha miradi iliyokusudiwa?,alihoji.

Akijibu swali hilo, Waziri Mkuu amesema Serikali ya awamu ya sita imepeleka fedha nyingi kwenye Halmashauri kwa ajili ya maendeleo. “Ni kweli Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepeleka fedha nyingi kwa ajili ya maendeleo na upelekaji huu ni wakati wote tangu mwanzo wa mwaka ili kuwafanya wananchi wapate maendeleo kupitia miradi inayolengwa.”

Amesema Serikali iliweka sheria ambayo inataka ifikapo tarehe 15 Juni ya mwaka wa fedha husika, kama Halmashauri haijamudu kumaliza fedha ilizopangiwa ni lazima fedha hizo zirudi.

“Utaratibu huo unazitaka Halmashauri zitoe taarifa kuwa wana kiasi cha fedha ambacho hakijatumika ni lazima waandike barua kuonesha kwamba hadi tarehe hiyo bado wana fedha kiasi gani, na zinasubiri utaratibu upi, waeleze majengo yamefikia linta au wanasubiri taratibu za manunuzi,” amesema.

Waziri Mkuu amesema sheria hiyo imewekwa kwa kuzingatia kuwa fedha hizo zinatoka kwa awamu kulingana na hatua za utekelezaji wa miradi.

 

 

     

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here