Home LOCAL WASAIDIENI WABUNIFU WACHANGA – WAZIRI MKUU

WASAIDIENI WABUNIFU WACHANGA – WAZIRI MKUU

DODOMA.

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameziagiza taasisi na mamlaka ambazo zinashiriki kuendeleza wabunifu wachanga zihakikishe zinawawezesha kubiasharisha ubunifu na uvumbuzi wao.
 
“Taasisi za sayansi na teknolojia; vyuo vikuu; taasisi za utafiti na maendeleo; na mamlaka mbalimbali kama SIDO, VETA na DON BOSCO ambazo kwa namna moja ama nyingine zinashiriki kuendeleza wabunifu wachanga ziwasaidie kubiasharisha ubunifu na uvumbuzi wao,” amesema.
 
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumanne, Mei 11, 2021) wakati akifunga maonesho ya Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU) yaliyofanyika katika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.
 
Amesema kuwa uendelezwaji wa wabunifu na wavumbuzi ufanyike kwa kasi na ufanisi mkubwa ili kuhakikisha matunda ya jitihada zinazofanywa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia za kuwaibua na kuwatambua wabunifu wachanga zinazaa matunda.
 
Nitoe wito kwa taasisi zote kutumia ubunifu na uvumbuzi unaozalishwa nchini kama nyenzo muhimu wakati wa kuandaa na kutekeleza mipango mbalimbali inayoandaliwa katika sekta zote, iwe za huduma au uzalishaji, ili kuongeza tija na kasi ya maendeleo ya Taifa letu” amesema.

Akielezea kuhusu suala la hatimiliki za wabunifu, Waziri Mkuu amesema anatarajia kuona mabadiliko ya haraka kwenye eneo hilo kwani hadi sasa idadi ya maombi yaliyowasilishwa kutoka Tanzania ni ndogo sana ikilinganishwa na maombi kutoka nchi jirani.
 
“Takwimu zilizotolewa na Shirika la Hatimiliki Duniani (World Intellectual Property Organization – WIPO) zinazoonesha kwa mwaka 2020, Tanzania iliwasilisha maombi ya hatimiliki nane tu, ikilinganishwa na nchi moja ya jirani iliyowasilisha maombi ya hatimiliki 372; na Afrika Kusini iliyowasilisha maombi ya hatimiliki 1,514. Idadi hii ni ndogo sana, ninatarajia kuona mabadiliko katika eneo hili, haraka sana.”

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here