Home BUSINESS NAIBU WAZIRI KIGAHE AFUNGUA MAONESHO YA SIDO, ASISITIZA WAJASIRIAMALI KUSAJILI BIASHARA ZAO...

NAIBU WAZIRI KIGAHE AFUNGUA MAONESHO YA SIDO, ASISITIZA WAJASIRIAMALI KUSAJILI BIASHARA ZAO BRELA MANYARA.

Naibu Waziri wa Wizara ya Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe (Mb), akipata maelezo mafupi kutoka kwa Afisa wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA)  Bw.Gabriel Girangay (katikati), kuhusu ushiriki wa BRELA katika maonesho ya SIDO Kanda ya Kaskazini, yanayofanyika katika viwanja vya Kwaraa, vilivyopo mjini Babati Mkoani Manyara. Maonesho haya yameanza tarehe 27 Mei hadi tarehe 31 Mei, 2021, karibu tukuhudumie.

Waziri Mkuu Mstaafu Bw. Fredrick Sumaye akisaini katika kitabu cha wageni katika banda la BRELA katika maonesho ya SIDO yanayofanyika katika viwanja vya Kwaraa, vilivyopo Mjini Babati, maonesho hayo yameanza jana tarehe 27 Mei na yatamalizika tarehe 31 Mei, 2021. Karibuni tuwahudumie.

Na: Christina Njovu, MANYARA.

Naibu Waziri wa Wizara ya Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe (Mb) amewataka wananchi na wajasiriamali katika Mikoa ya Manyara, Arusha, Kilimanjaro na Tanga kutembelea katika mabanda ya washiriki wa maonesho ya SIDO kanda ya Kaskazini yanayofanyika katika viwanja vya Kwaraa mjini Babati ili kupata huduma zinazotolewa na washiriki wa maonesho hayo ikiwemo Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni BRELA. 

Mhe. Kigahe amesema hayo alipokuwa akifungua maonesho ya SIDO kanda ya kaskazini yanayofanyika katika viwanja vya Kwaraa vilivyopo Mjini Babati Mkoani Manyara wakati akitembelea mabanda ya washiriki wa maonesho hayo na kuzungumza na baadhi ya wajasiriamali ambao wamemuomba kusaidia kutatua changamoto wanazokabiliana nazo na kusaidia kuharakisha upatikanaji wa huduma ambazo wanazihitaji zikiwemo  kusajili biashara zao, kupata nembo za ubora na pia kupata huduma mbalimbali zinazotolewa na Taasisi za umma. 

“Tembeleeni maonesho haya ili muweze kujifunza na kufahamu umuhimu wa kusajili Majina ya Biashara na Makampuni pia mtaweza kusajili Majina ya Biashara na Makampuni yenu hapa hapa uwanjani katika banda la Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni BRELA ambao nao ni miongoni mwa washiriki katika maonesho haya.  Pia mtaweza kujua mbinu za kutafuta masoko ya bidhaa, fursa za masoko zilizo wazi nchini  na mikakati ya kushiriki maonesho mbalimbali yanayoandaliwa na SIDO na mashirika mengine” amesema Mhe. Kigahe.

Aidha ameongeza kuwa wajasiriamali wakiweza kupata mafunzo hayo hivi sasa yatawawezesha kupata ushiriki wa kimkakati kwakuwa yatawawezesha kushiriki katika maonesho mbalimbali ya kitaifa na kimataifa kwakuwa suala la kufanya Biashara ni endelevu na linahitaji elimu kila wakati na kuwasihi wafunguke  na waendelee kutafuta elimu hususani kutoka shirika la viwanda vidogo SIDO ili Biashara zao zizidi kukua. 

Awali Mhe. Naibu Waziri Kigahe alitembelea banda la Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni  BRELA ambalo ni miongoni mwa mabanda ya washiriki katika maonesho hayo alipata maelezo juu ya sababu ya  ushiriki wa wakala katika maonesho hayo kutoka kwa  Afisa Usajili wa Wakala wa Biashara na Leseni (BRELA) Gabriel Girangay  ambaye amemueleza Naibu Waziri Mh.Exaud Kigahe  kuwa;

“BRELA imeshiriki katika maonesho ya SIDO kanda ya Kaskazini ili kusogeza huduma zetu karibu, huduma zetu zinatolewa kwa njia ya mtandao   huduma hizo ni  pamoja na Usajili wa Makampuni, Usajili wa Majina ya Biashara, Usajili wa Alama za Biashara na Huduma”.  

Girangay aliongeza kuwa; “Vile vile tunatoa Hataza ambayo ni hati miliki Ubunifu, Utoaji wa Leseni za Biashara kundi A, Utoaji wa Leseni za Viwanda”.    

Ushiriki huu unatoa fursa kwa Wananchi wa Mkoa wa mikoa ya Manyara, Arusha, Kilimanjaro na Tanga wanaohitaji kupata sajili mbali mbali ama waliokuwa wakipata changamoto za kufanya sajili kwa njia ya mtandao kuweza kupata  huduma moja kwa moja. 

Maonesho haya yaliyoanza jana tarehe 27 Mei yanatarajiwa kufungwa tarehe 31 Mei ,2021 yanawakutanisha wananchi wa mikoa ya Manyara, Arusha, Kilimanjaro na Tanga.

BRELA inawakaribisha wananchi wote  kutembelea banda lake ili waweze kuhudumiwa. 

‘BRELA tunaipa utu wa kisheria biashara yako’. 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here