Home LOCAL HEDHI ISIWE CHANZO CHA MAAMBUKIZI YA MAGONJWA.

HEDHI ISIWE CHANZO CHA MAAMBUKIZI YA MAGONJWA.

Na: WAMJW-Dodoma

Imebainishwa kuwa hedhi salama inatakiwa kuzingatiwa na msichana au Mwanamke ili kuepuka maambukizi ya magonjwa.

Hayo yamesemwa leo na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bi. Mwanaidi Khamis kwa niaba ya Waziri Dkt. Dorothy Gwajima katika kilele cha maadhimisho ya siku ya hedhi salama duniani ambayo yamefanyika jijini Dodoma.

Naibu Waziri huyo amesema lengo kuu la maadhimisho hayo duniani ni kuelezea umma wa watanzania kuwa hedhi sio ugonjwa wala laana bali ni hali ya kawaida inayomtokea msichana au mwanamke katika mfumo wa uzazi mara baada ya kufikia umri wa balehe.

“Ni wakati mzuri wa kuelewa na kuibua changamoto zinazowakabili wasichana na wanawake wakati wa hedhi na namna bora ya kuzitatua ili kuepuka magonjwa kwa kuzingatia usafi wa mwili. Tafiti zinaonesha kuwa kila siku wanawake Zaidi ya milioni 12 wenye umri kati ya miaka 15 na 49 wanakuwa kwenye hedhi”. Amesema Bi. Mwanaidi.

Bi. Mwanaidi ameongeza kuwa hedhi salama ni muhimu kwa afya, maendeleo na utu wa msichana na mwanamke kuanzia shule za msingi mpaka vyuo Pamoja na wale waliopo nyumbani wanahitaji upatikanaji wa huduma za hedhi salama bila kuwa na vikwazo.

“Ni Dhahiri kwamba wasichana na wanawake katika nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania wanakabiliwa na changamoto za mazingira yasiyo Rafiki wakati wa hedhi hususan upatikanaji wa maji safi na salama, vyoo bora vyenye chumba cha kubadilishia taulo za kike, sehemu za kunawa mikono na dhana za kutimika kuteketeza vitambaa vya hedhi vilivyotumika”. Amesema Naibu Waziri Mwanaidi.

Aidha, Naibu Waziri huyo ametoa wito kwa jamii kuchukua hatua kuondokana na baadhi ya changamoto ili kusaidia wasichana na wanawake kunyanyapaliwa au kutengwa kutokana na hali ambayo wameumbwa nayo.

Maadhimisho ya siku ya hedhi salama mwaka huu yameongozwa na kaulimbiu isemayo “Ni wakati wa kuchukua hatua ili kuhakikisha vifaa vya kujisitiri/tauro za hedhi zinapatikana kwa urahisi na kwa bei nafuu msichana/mwanamke”.

Mwisho
Previous articleWAJASIRIAMALI WENGI HAWANA MAWAZO MAPYA YA KIBIASHARA KUTOKANA NA KURIDHIKA NA WANACHOKIUZA: PROF. MJEMA
Next articleNAIBU WAZIRI KIGAHE AFUNGUA MAONESHO YA SIDO, ASISITIZA WAJASIRIAMALI KUSAJILI BIASHARA ZAO BRELA MANYARA.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here