DAR ES SALAAM.
Mkuu wa Wilaya ya Ilala Ng’wilabuzu Ludigija amewataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Uviko -19 na kufuata miongozo ya Afya iliyopo uliyotolewa na wataalam.
Mheshimiwa Ludigija aliyasema hayo katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika katika ukumbi wa Anatoglo ambapo amesema kuwa ni vema wananchi wakazidi kuchukua tahadhari zote za kujikinga na ugonjwa huo.
“Nitoe maelekezo kwa kamanda wetu wa Mkoa wa kipolisi Ilala aweze kuwasimamia Askari wa usalama Barabarani ili kuangalia magari kuweza kufuata maelekezo yaliyotolewa lengo ni kuhakikisha kuwa tunajikinga katika kipindi hiki ambacho ugonjwa upo hivyo tunataka kuona wananchi wanachukua tahadhari zote” alisema Ludigija.
Aidha Mkuu huyo wa wilaya ameendelea kusisitiza wananchi kuhepuka mikusanyiko isiyo ya lazima isipokuwa kwenye shughuli muhimu kama misiba ama harusi na kusiwe na idadi kubwa ya watu nakwamba taadhari zote zichukuliwe ikiwemo kukaa umbali wa mita moja ili kuendelea kujikinga.
“kwenye maswala ambayo yatahusisha mkusanyiko mkubwa tunaomba Ofisi yetu ya Mkurugenzi au Mganga Mkuu wa Mkoa washiriki kutoa vibali maalumu ili kujiridhisha juu ya shughuli mbalimbali za wananchi zinafata taratibu zailizopo” aliongeza.
Mkuu wa Wilaya Pia amezungumzia suala la chanjo ya ugonjwa wa Uviko-19 na kufafanua juu ya uvumi unaoenezwa mashuleni kwamba kuna watoto wanaolazimishwa kuchanja na kwamba uvumi huo hauna ukweli na wala jambo hilo halipo kwani yapo maelezo yaliyotolewa yanayoeleza ni aina gani ya watu wanaopaswa kuchanja na kwamba chanjo hiyo ni hiyari.
Aliongeza kuwa Mheshimiwa Rais alishaelekeza juu ya utoaji wa chanjo hiyo na watu wanatakiwa kuchanja na kueleza kuwa watoto hawatapata chanjo hiyo hivyo ni vema wananchi wakafahamu hilo na kuachana na uvumi wa watu wenye nia ovu juu ya chanjo hiyo.