DAR ES SALAAM
Naibu Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe, amewahimiza Watanzania kutumia kwa usahihi Falsafa ya Kaizen katika maeneo ya kazi ili kutimiza malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa pamoja na azma ya Serikali ya Awamu ya Sita inayodhamiria Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa juu wa kati unaoongozwa na ukuaji wa sekta ya viwanda.
Kigahe ameyasema hayo, alipokuwa Akimwakilisha Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dk Ashatu Kijaji katika ufunguzi wa Maadhimisho ya Tatu ya Siku ya Kaizen Tanzania ambayo yalijumuisha utoaji wa tuzo kwa viwanda vilivyoshinda katika Mashindano ya 6 ya Kaizen kwa viwanda vinavyotekeleza falsafa hiyo, yaliyofanyika Februari 10, 2022 Dar es salaam .
Aidha, ameiomba Serikali ya Japan kupitia kwa Balozi wa Japan nchini Tanzania, MShinichi Goto, kuendelea kufadhili mradi wa Kaizen ili kusambaza falsafa hiyo kuendana na utekelezaji wa Mpango wa Kitaifa wa Miaka 10 – “FKM 2020-2030” wa kueneza falsafa ya Kaizen pamoja na kufikia hatua ya kuunganisha magari ya Japan nchini Tanzania.
“Japan na Tanzania ni marafiki, sasa twende zaidi ya hapo; kwa kuwa sisi ndio wateja wenu wakubwa wa magari na Tanzania tumefikia uchumi wa kati. Ni muda mwafaka sasa sekta binafsi ya Tanzania na sekta binafsi ya Japan kufanya uunganishaji wa magari hapa nchini,” alisema Naibu Waziri na kuwasisitiza Watanzania kujiandaa vema kwa hilo kwa manufaa ya nchi zote mbili.
Kigahe pia aliwashauri Watanzania kuzingatia ubora na kujikita katika ushindani ili Tanzania isiwe tu soko la bidhaa za nchi nyingine, bali Watanzania washiriki kwa viwango vya ubora wa hali ya juu katika soko likiwamo Eneo Huru la Biashara Afrika.
Akizungumza katika ufunguzi wa maadhimisho hayo yenye Kaulimbiu isemayo: “Kaizen! Kwa Tanzania ya Viwanda na Maendeleo Jumuishi!” Balozi wa Japan nchini Tanzania, MShinichi Goto, alipongeza Tanzania kwa kukua kiuchumi licha ya changamoto zilizotokana na Covid-19 na kuitaka kutilia mkazo maendeleo ya biashara na viwanda vidogo na vya kati ili kukuza uchumi.
Naye Mwakilishi Mkazi Mkuu wa JICA nchini Tanzania, Naofumi Yamamura, alisema tangu Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Bishara na JICA zishirikiane kutekeleza falsafa ya Kaizen, mwaka 2013 kuimarisha sekta ya viwanda, zaidi ya kampuni 100 nchini zinatekeleza falsafa hiyo na Watanzania 150 wamefuzu kuwa wakufunzi wa Kaizen.