Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) amewaasa wananchi wa Kitongoji cha Nkanka ,Kijiji cha Itumba katika Halmashauri ya Wilaya ya Ileje Mkoani Songwe, kuheshimu maeneo yatakayobaki baada ya kumegewa sehemu ya Hifadhi ya Msitu wa Ileje Range baada ya mipaka kuwekwa.
Amesema hayo leo wakati wa ziara ya Kamati ya Mawaziri wa Kisekta ya Kutatua migogoro ya ardhi wilayani humo.
Amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameridhia Kitongoji cha Nkanka kumegewa sehemu ya hifadhi na kuwataka wananchi kuacha kuendelea kuvamia eneo la msitu huo kwa ajili ya matumizi yao binafsi.
“Sasa niwaombe huruma ya Mheshimiwa Rais isije ikawafanya mkajisahau, ninyi sasa hivi mtakuwa sehemu ya hifadhi mtasimamia na kuhakikisha miti haichomwi, haikatwi hovyo na shughuli za kibinadamu haziingii kwenye eneo hili la hifadhi” amesisitiza.
Amesema ni lazima kulihifadhi eneo hilo na kulisimamia lisiingiliane na shughuli za kibinadamu ili kutunza mazingira ili kudhibiti mabadiliko ya tabia ya nchi yanayopelekea kuwepo kwa ukame.
Amefafanua kuwa baada ya wataalamu kutoka Wizara ya Ardhi, Wizara ya Maliasili na Utalii, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa kushirikiana na wananchi wa Nkanka, kufanya marudio ya kutambua na kuweka vigingi wananchi hawataruhusiwa kuingia tena ndani ya hifadhi hiyo.
Amewataka wananchi hao kusimamia vizuri eneo watakalopewa kwa kupanga matumizi bora ya ardhi na kufanya shughuli zao za kilimo na ufugaji katika eneo hilohilo.
Awali akizungumza na watendaji wa Mkoa wa Songwe, Mhe. Masanja amewaomba kuendelea kutatua migogoro ya mipaka na uvamizi wa maeneo ya hifadhi ili kumsaidia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kutekeleza majukumu mengine ya kitaifa.
Ziara ya Kamati ya Mawaziri wa Kisekta imehitimisha ziara katika Mkoa wa Songwe na itaendelea katika Mkoa wa Mbeya Oktoba 24,2022.