Meneja Msadizi Akiba ya Fedha za Kigeni wa Benki kuu ya Tanzania (BoT) Dr Anna Lyimo akielezea namna Benki Kuu ya Tanzania ilivyojipanga Kwa ajili ya kuanza kununua Madini Kwa wachimaji nchini.
Meneja Msadizi Akiba ya Fedha za Kigeni wa Benki kuu ya Tanzania (BoT) Dr Anna Lyimo akitoa elimu Kwa wananchi waliotembelea Katika Banda la Taasisi hiyo kwenye maonesho ya 5 ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika Viwanja vya EPZA Bombambili mkoani Geita.
Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inatarajia kuanza kununua madini ya dhahabu kutoka kwa wachimbaji nchini hivi karibuni.
Hayo yameelezwa na Meneja Msadizi Akiba ya Fedha za Kigeni wa Benki kuu ya Tanzania Dkt. Anna Lyimo katika maonesho ya 5 ya Teknolojia ya Madini mkoani Geita ambapo amesema Benki kuu ina wajibu wa kisheria wa kuhifadhi akiba ya fedha za kigeni hapa nchini.
Amesema Benki kuu imefanya tafiti mbalimbali kupata vyanzo kuweza kuongeza akiba ya fedha za kigeni, ambapo mojawapo ya tafiti iliyofanywa ni baada ya mabadiliko na maboresho katika sheria ya madini na sekta ya madini kwa ujumla, uanzishwaji wa viwanda vya kuchenjulia dhahabu, pamoja na kukua kwa teknolojia ya kupima viwango vya dhahabu ambavyo vyote kwa pamoja vimesaidia kuongeza kiwango cha fedha za kigeni hapa nchini
Ameongeza kwamba madini hayo yatanunuliwa hapa nchini kwa fedha za kitanzania na baadae kupelekwa nje ili kuongezewa thamani ili yaweze kuthibitishwa katika viwango vya kimataifa na kuhifadhiwa katika masoko ya kimataifa kwa kutumia fedha zetu za kigeni zilizopo nchi za nje .
Ameeleza faida mbalimbali zitakazopatikana kwa kununua dhahabu nchini ikiwa ni kuongeza kiwango cha akiba ya fedha za kigeni kwa bei nafuu, pamoja na kuisaidia serikali kupunguza kiwango cha mikopo ambayo serikali ingetakiwa kukopa ili kuongeza akiba ya fedha za kigeni.
Ameongeza kuwa faida nyingine ya kununua dhahabu nchini ni kuipatia sekta ya madini soko la uhakika ambapo wachimbaji wadogo wadogo na wachimbaji wakubwa wa madini badala ya kwenda kuuza madini yao soko la nje wanaweza kwenda benki kuu kuuza madini yao kwa bei nzuri na ya uhakika ambapo itawapunguzia gharama za kwenda nje ya nchi.
Amehitimisha kwa kusema Benki kuu itatoa taarifa kwa wananchi kuhusu tarehe rasmi ya kuanza kununua madini ya dhahabu nchini.