Na :Mwandishi wetu, Mtwara
VIONGOZI mbalimbali wa mkoa wa Mtwara wameweka wazi kwa kubariki ujio wa pambano la Mtwara Ubabe Ubabe 2 huku wakazi wa Naliendele nje ya mji mkoani hapa wakifurahia zoezi la uzwaaji wa tiketi wa pambano hilo.
Katika pambano hilo ambalo linatarajia kufanyika Septemba 24, mwaka huu kwa bondia Mtanzania, Twaha Kiduku atapanda ulingoni kutetea mkanda wa ubingwa wake wa UBO dhidi ya Abdo Khaled wa Misri katika pambano la raundi kumi litakalopigwa kwenye Uwanja wa Nagwanda Sijaona uliopo mkoani hapa.
Mwenyekiti wa CCM mkoani wa Mtwara, Yusuph Nanila alisema kuwa uwepo wa pambano hilo utafungua fursa nyingi za kiuchumi huku akisisitiza imani yake kubwa ipo kwa Twaha Kiduku kushinda pambano hilo katika raundi za mapema kutoka na historia ya wapigania uhuru iliopo mjini hapa.
“Hili siyo pambano la kawaida ni pambano la kimataifa ambalo sisi wana Mtwara tumefaidika nalo kwa mambo mengi kutokana na kufanyika kwa mara ya kwanza, nitoe wito kwa wana Mtwara, Ruvuma na nchi za jirani waje waangalie pambano kwa sababu naamini Kiduku atashinda mapema maana hakuna aliyewahi kushondwa hapa,” alisema Nanila.
Wakati huohuo wakazi wa Naliendele waliopo nje ya Mtwara, mjini wamepongeza zoezi la uzwaaji wa tiketi wa kuelekea katika pambano kutokana na watu wengine wakiwa wamejikatia tayari kushuhudia pambano hilo.
Baadhi ya wakazi hao walinunua tiketi hizo ni Seleman Oga, Jackson Constantini na Zena Salum ambao wote wamepongeza pamoja na kuhamasisha wakazi wengine wa mjini hapa kukata tiketi zao mapema zinazouzwa kwa bei Sh 5000, Sh 10,000 na Sh 20,000.