Makamu wa kwanza wa Rais Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman akizungumza wakati wa kufunga rasmi Kongamano la Wanawake na Vijana lililofanyika kwa siku tatu Jijini Dar es Salaam chini ya Sekretarieti ya Eneo Huru la Biashara Afika.
Makamu wa kwanza wa Rais Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman akizungumza (kulia) akizungumza na Katibu Mtendaji wa Sekretarieti ya Eneo Huru la Biashara Afrika Wamkele Mene (kushoto) mapema kabla ya kufanyika hafla ya kufunga rasmi Kongamano hilo.
Na: Hughes Dugilo, DAR ES SALAAM.
Makamu wa kwanza wa Rais Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman amesema kuwa ushirikishwaji wa wanawake na vijana ngazi mbalimbali ikiwemo nafasi za uwakilishi ni hatua moja wapo muhimu itakayochochea ufanisi katika Biashara zinazoendeshwa na kundi hilo barani Afrika.
Ameyasema hayo Septemba 14 2022 Jijini Dar es Salaam alipokuwa akimuwakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi , Dkt. Hussein Ali Mwinyi wakati akifunga Mkutano wa Wanawake na Vijana katika Biashara chini ya Mkataba wa Eneo Huru la Biashara Africa.
Amesema kuwa ni imani yake kwamba katika siku tatu za mkutano huo wameweza kujadili kwa pamoja namna ya kutatua changamoto zinazowakabili wanawake na vijana wa Afrika zitakazowasaidia kufanya Biashara katika mazingira yanayofaa.
Aidha amesema kuwa anatarajia kuona maazimio yote yaliyofikiwa katika mijadala waliyofanya yatafanyiwa kazi na Secretariat ya AfCFTA kwa kuahirikiana na nchi wanachama.
“Maazimio haya yatakuwa msingi na yataleta hamasa ya ushiriki wa wanawake na vijana wengi zaidi katika shughuli mbalimbali za Biashara katika Bara la Afrika na Duniani kwa ujumla”
“Ni matumaini yangu pia kuwa katika mkutano huu yamepatikana mapendekezo mahususi ambayo yatasaidia katika uandaaji wa itifaki ya wanawake na vijana ambayo inategemewa kuwainua wanawake na vijana katika Biashara chini ya Eneo Huru la Biashara la Afrika”
Katika hatua nyinge mhe. Othman amezipongeza na kuzishukuru nchi zote za Afrika kwa heshima kubwa waliyoipatia Tanzania na kumuamini Rais WA Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na kumteua kuwa Kinara na Mhamasishaji wa wanawake na Vijana katika Biashara Afika.
“Ninawahakikishia kuwa hamkukosea kwa kuamini kuwa Mheshimiwa Rais Samia atatekeleza kwa umahiri mkubwa jukumu hilo la kuwahamasisha wanawake na vijana katika Biashara Barani Afrika kwa kuwa ana ushawishi na uzoefu katika masuala ya Maendeleo” amesema.