Afisa Sheria kutoka Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Bw. AbdulKarim Nzori (kulia) akieleza namna Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), inavyotekeleza majukumu yake kwa Mhe. Balozi Lt. Gen. (Rtd) Anselem Nhamo Sanyatwe, Balozi wa Zimbabwe nchini Tanzania (Mwenye suti ya Bluu) na Mhe. Balozi Andrew Zumbe Kumwenda, Balozi wa Malawi nchini Tanzania (Mwenye suti ya kijani), walipotembelea banda la BRELA kwenye maonesho ya Mara Business Expo 2022 yanayoendelea mkoani Mara.
Mhe. Balozi Lt. Gen. (Rtd) Anselem Nhamo Sanyatwe, Balozi wa Zimbabwe nchini Tanzania na Mhe. Balozi Andrew Kumwenda, Balozi wa Malawi nchini Tanzania wamefurahishwa na namna Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) inavyosaidia wawekezaji wanaokuja nchini Tanzania.
Pongezi hizo zilitolewa baada ya kupewa taarifa namna BRELA inavyotoa huduma na kusaidia wawekezaji ndani ya kituo cha huduma ya pamoja katika ofisi ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).
Bw. Abdulmalik Azori Afisa Sheria aliwaeleza Mabalozi hao kuwa BRELA imeweka dawati TIC ambapo kila mwekezaji anayekuja nchini anapewa huduma kwa karibu na usaidizi wa haraka ili kuanza biashara bila kikwazo chochote.
“BRELA ni lango la kila mwekezaji anayekuja nchini kufanya biashara maana atahitajika kwanza kuomba leseni za biashara”, ameeleza Bw. Nzori
Naye Mhe. Balozi Lt. Gen. (Rtd) Anselem Sanyatwe amesema kuwa amefurahishwa kusikia kuwa mwekezaji yeyote nchini anapata huduma zote za BRELA ndani ya siku tatu baada ya ukamilishaji wa nyaraka zote.
Mabalozi hao walitembelea banda la BRELA kwenye Maonesho ya Mara Business Expo 2022 yanayofanyika Musoma mkoani Mara.