IMEELEZWA kwamba, Nape Nnauye ambaye ni Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ana dhamira njema na tasnia ya habari, lakini dhamira yake haijalindwa na sheria za tasnia hiyo.
Ni kauli ya Deodatus Balile, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), akizungumza katika Kipindi cha Jambo kinachorushwa na Kituo cha Televisheni cha TBC1 tarehe 11 Agosti 2022.
Amesema, dhamira ya Nape ya kutotaka kuoana kosa la mwandishi linagharimu chombo cha habari ipo wazi, lakini bado sheria ina dhamira kinyume na dhamira yake.
“Waziri Nape katuelewa lakini hauwezi kusema deal done (kazi imekwisha). Tunamshukuru sana kwani ameonesha dhamira njema katika kuhakikisha kosa la mwandishi haliathiri chombo cha habari.
“Tumeona ameshughulikia kuvitoa vyombo vya habari vilivyokuwa kifungoni, tunaamini ana dhamira njema lakini bado sheria ni zile zile ambazo zikitumika, maafa ni yake yake,” amesema Balile.
Pia amesema, mwandishi wa ahabari anapoteleza katika uandishi wake, hapaswi kupelekwa mahakama kama ilivyo taaluma zingine nchini bali anapswa kushtakiwa kwenye bodi ya taaluma yake.
“Kosa la kitaaluma halipelekwi mahakamani, unampelekaje mahakamani mtu kwa kosa la kitaaluma? Ndio maana tunasema kuwepo na chombo ambacho kitasimamia tasnia kama ilivyo kwenye taaluma zingine.
“Mwanasheria akifanya kosa, serikali haimsimamishi bali chombo nadani ya taaluma yake ndio kinamsimamisha ama kumpa adhabu, hivyo hivyo kwa daktari na hata wahandisi lakini kwanini waandishi ndio wahukumiwe (na serikali) moja kwa moja?” amehoji.
Pia Balile amesema, wadau wa habari nchini wanataka sheria katika tasnia hiyo zitoe mwongozo wa kukuwa kwa uhuru wa habari na sio kudhibiti habari na wanahabari.
“Rais Samia (Suluhu Hassan) tulipokutana naye, alisisitiza anataka sheria zirekebishwe na ziwe bora. Tunaamini tutajadili na tutakubaliana ili tuwe na sheria zinazokubalika kimataifa,” amesema.