Home BUSINESS WAFANYABIASHARA WENGINE WATATU WAPANDISHWA KIZIMBANI KWA KUSHINDWA KUOMBA KUSAJILIWA NA KODI YA...

WAFANYABIASHARA WENGINE WATATU WAPANDISHWA KIZIMBANI KWA KUSHINDWA KUOMBA KUSAJILIWA NA KODI YA ONGEZEKO LA THAMANI VAT.

NA: FARIDA SAID, MOROGORO.

MAMLAKA ya Mapato nchini TRA Mkoa wa Morogoro imeendelea kuwapandisha kizimbani wafanyabiashara wanaodaiwa kushindwa kutii sheria ya usimamizi wa kodi na sheria ya kodi ya ongezeko la thamani VAT licha ya makusanyo yao kwa mwaka kuwa ni zaidi ya shilingi milioni mia moja na kutajwa kwenye sheria.

Mamlaka hiyo leo Septemba mosi imewafikisha mahakamani wafanyabiashara watatu wilayani Mvomero mkoani hapa wakikabiliwa na mashitaka matatu ,likiwemo la kushindwa kuomba kusajiliwa na kodi ya ongezeko la thamani VAT.

AMBAPO waliopandishwa kizimbani ni kampuni ya mafleta farm LTD Ikiwakilishwa na mkurugenzi wake Ahmad Yahya ,Naiman Biniely Chau na Timoth Matemba ambaye hakutokea mahakamani hapo na Mahakama kutoa hati ya kumkamata na kumfikisha Mahakamani hapo Septemba 08 kesi hizo zitakapofikishwa tena kwa usikilizwaji wa awali.

Mbele ya hakimu wa Mahakama ya wilaya ya Mvomero, Asha Hassan Waziri, ilidaiwa na mwendesha mashitaka mwandamizi wa Serikali Cherubini Chuwa kuwa washtakiwa hao walitenda makosa hayo kwa nyakati tofauti katika kipindi cha Julai mwaka huu.

Washtakiwa hao wanadaiwa kushindwa kuomba kusajiliwa kwenye kodi ya ongezeko la thamani VAT, kinyume kifungu 28 cha sheria ya kodi ya VAT sura 148, ikisomwa pamoja na kifungu Cha 90 (1) cha sheria ya usimamuzi wa kodi namba 10 ya mwaka 2015 yenye marejeo hadi mwaka 2019.

Shtaka la pili ni kuwazuia maafisa wa TRA kufanya kazi yao kwa kukataa kwa makusudi kurejesha fomu za VAT walizopewa, kinyume na kifungu cha 85 (3) (I) cha sheria ya usimamuzi wa kodi namba 10.

Aidha shitaka la tatu ni kwa washtakiwa hao kushindwa kuendana na matakwa ya sheria ya kodi kwa kitendo cha kutofika kwa hiyari kusajiliwa kwenye Kodi ya VAT kinyume na kifungu cha 28 cha sheria ya Kodi, kikisomwa pamoja na kifungu cha 82 cha sheria ya usimamizi wa kodi.

Hata hivyo washitakiwa hao wote walikana mashitaka huku mahakama ikiweka wazi masharti ya dhamana kwa kutaka washitakiwa kila mmoja kuwa na wadhamini wawili watakaokuwa na barua za utambulisho na kusainj hati ya dhamana ya shilingi milioni mbili.

Mwendesha mashtaka huyo mwandamizi wa Serikali alisema upelelezi wa Mashauri hayo umekamilika na yatafikishwa tena Mahakamani hapo Septemba 08 mwaka huu  kwa usikilizaji wa awali.

Ikumbukwe kuwa hivi Karibuni mahakama hakimu mkazi wilaya ya Kilosa iliwafikisha Mahakamani washtakiwa sita, Kibwana Kidinilo, Kitete Sugar, Clement Gwila na Mathias Mligwa pamoja na Gajoki LTD na Green Line Brothers ambao hawakutokea Mahakamani mbele ya hakimu mkazi mfawidhi Agnes Ringo wakidaiwa kutenda makosa yanayofanana na hayo mnamo Julai 26 kwa nyakati tofauti.

Mwisho.

Previous articleSERIKALI ITAENDELEA KUCHUKUA HATUA MADHUBUTI KUHAKIKISHA NHIF INAZIDI KUIMARIKA: UMMY MWALIMU
Next articleKINANA AKAGUA MRADI UJENZI WA GATI LA BANDARI YA UJIJI MKOANI KIGOMA
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here