Home LOCAL ZAIDI YA SH. BILIONI 28 KUJENGA KITUO CHA UPANDIKIZAJI FIGO TANZANIA

ZAIDI YA SH. BILIONI 28 KUJENGA KITUO CHA UPANDIKIZAJI FIGO TANZANIA

▪️Ni kikubwa katika Ukanda wa Jangwa la Sahala_

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

▪️Pia itatumika katika kutoa mafunzo kwa madaktari bingwa_

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ameshuhudia utiaji saini wa hati ya makubaliano ya ujenzi wa kituo kikubwa cha kupandikiza figo pamoja na utoaji mafunzo kwa madaktari bingwa ambacho kitakuwa ni kikubwa katika ukanda wa Jangwa la Sahara.

Kituo hicho ambacho kitajengwa kwenye Hospitali ya Kanda ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma ni ushirikiano kati ya Shirika la Tiba la TOKUSHUKAI, Hospitali ya Benjamin Mkapa na Chuo Kikuu cha Dodoma na kinatarajia kugharimu zaidi ya shilingi bilioni 28 ikiwa ni msaada usiokuwa na masharti yoyote.

Utiaji saini huo umefanyika jana (Jumatatu, Mei 26, 2025) wakati kongamano la Biashara, Uwekezaji na Utalii lililowakutanisha wafanyabiashara wa Tanzania na wafanyabiashara na wawekezaji wa Japan katika ukumbi wa mikutano wa Hoteli ya Westin, Osaka, Japan, ikiwa ni sehemu ya ushiriki wa Tanzania katika maonersho ya World Expo Osaka 2025. Kongamano hilo lilifunguliwa na Mheshimiwa Majaliwa.

Akizungumza baada ya utiaji saini huo Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamini Mkapa, Profesa Abel Makubi amesema wamesaini makubaliano na shirika hilo linaloundwa na kundi la madaktari Wakijapan ambao wamekuwa wakisaidia utoaji na uboreshaji huduma za afya. “Hawa ni wadau wetu wa muda mrefu na walikuwa watu wa kwanza kusaidia utoaji wa huduma Dialysis katika hospitali ya Benjamin Mkapa.”

“MOU hii ambayo tumeisaini sasa hivi ni kwa ajili ya kujenga kituo cha umahiri katika upandikizaji figo kwenye eneo la Tanzania na Ukanda wa Jangwa la Sahara.”

Amesema mbali na ujenzi wa kituo hicho ambacho kitajengwa ndani ya hospitali ya Benjamin Mkapa na kutarajiwa kukamilika na kuanza kutoa huduma ndani ya miaka mitatu, pia Serikali ya Tanzania imejipanga kusaidia baadhi ya maeneo ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati. Ujenzi wa kituo hicho unarajiwa kuanza mwaka huu.

“Tunatoa shukurani kwa Serikali ya Japan kupitia wadau hao na tunamshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira wezeshi ambayo yametufanya sisi tuweze kufikia makubaliano na wadau hawa. Makubaliano haya yanakwenda kusaidia wananchi kwa ajili ya kuboresha huduma za figo si kwa Watanzania tu bali kwa Waafrika wengine.”

Profesa Makubi amesema pia kituo hicho kitakuwa kinatoa mafunzo kwa ajili ya kupandikiza figo, pamoja na kufanya tafiti kwa ajili ya kuzuia au kupunguza magonjwa yanayohusiana na figo. Mafunzo yatolewa kwa ushirikiano kati ya Hospitali ya Benjamin Mkapa kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).

Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Profesa Lugano Kusiluka amesema makubaliano hayo yataimarisha huduma ya upandikizaji figo ambao unafanyika katika Hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma kwa ushirikiano wa wataalamu wa hospitali hiyo pamoja na wa UDOM.

Amesema kwa sasa UDOM ipo katika mchakato wa kuanzisha programu ya uhandisi wa vifaa tiba ili kuounguza gharama kwa Serikali kutumia wataalam kutoka nje ya nchi kutengeneza vifaa hivyo mara vinapoharibika. “Kwa makubaliano haya mbali na kufundisha wataamu kutengeneza vifaa hivyo, pia watafundisha namna ya kuvitunza ili visiharibike.”

Pia, Profesa Kusiluka amesema katika makubaliano hayo Tanzania inakwenda kunufaika kwa kuwa kituo kikubwa cha upandikizaji figo inachotarajiwa kujengwa kitatumika katika kufundisha madaktari bingwa pamoja na wataalam kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika kupandikiza figo na baadae kupandikiza viungo vingine.

Hati nyingine iliyosainiwa ni kati ya ushirikiano kati Chuo Kikuu cha Dodoma na Hospitali ya Benjamin Mkapa na Chama cha Maendeleo na Uchumi Afrika cha Japan (AFRECO), hati hizo ni sehemu ya hati sita za makubaliano zilizosainiwa leo kati ya Serikali Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na mashirika ya Japan.