Home BUSINESS FCC YAJIDHATITI KUTOA HUDUMA ZAKE KIDIGITALI

FCC YAJIDHATITI KUTOA HUDUMA ZAKE KIDIGITALI

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

Na: Mwandishi wetu, DSM

Tume ya Ushindani (FCC) inatarajia kuanza kutoa huduma zake kwa njia ya mtandao, itakayosaidia kurahisisha shughuli zake na kuwafikia wananchi kwa urahisi na haraka zaidi.          

Aidha, hatua hiyo itasaidi kutekeleza mradi mkubwa wa kiotomatiki utakaobadilisha mifumo ya uendeshaji wa Taasisi hiyo kuwa ya kidijitali, na kufanyakazi kisasa na kwa ufanisi.

Akizungumza mbele ya waandishi wa habari katika kikao kazi cha kumtambulisha Mkandarasi atakayetengeneza Mfumo huo, Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Bw. William Erio. ameeleza kuwa mradi huo unatekelezwa kwa msaada wa dola za Marekani 600,0000 kwa ufadhili wa Shirika la TradeMark Africa (TMA), nakwamba Kampuni ya Teknolojia ya hapa nchini, ICT-PACK, imechaguliwa kutekeleza kazi hiyo.

“Mradi huu, utakapozinduliwa, utabadilisha shughuli kuu za FCC kama usimamizi wa mashauri na ufuatiliaji wa uzingatiaji wa sheria kuwa katika mfumo wa kidijitali na kiotomatiki” amesema Erio.

Erio ameeleza Mradi huo ni wa miaka miwili, nakwamba takribani asilimia 75 ya maandalizi ya awali yamekamilika, huku akitoa matumaini kuwa muda wa utekelezaji unaweza kufupishwa kutokana na umuhimu wa kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia.

“Katika Dunia ya leo ya teknolojia inabadilika haraka, miaka miwili na nusu inaweza kutufanya tuwe tumepitwa. Napendelea mradi huu ukamilike mapema ili FCC ianze kufaidika mapema na mifumo hii” amesema. “Natoa wito kuongeza saa za kazi inapobidi na kufanya vikao vya kiufundi mara kwa mara ili kuharakisha hatua—bila kuathiri ubora” amesisitiza.

Aidha, ameongeza kuwa msaada wa Dola 600,000 kutoka TMA unapunguza mzigo mkubwa wa kifedha kwa serikali na kuiwezesha FCC kuendelea kutekeleza majukumu yake ya kisheria kwa ufanisi.

“Fedha hizi ambazo FCC ingetakiwa kuzitafuta kutoka serikalini. Sasa badala yake, tunaweza kuelekeza rasilimali hizo kwenye mahitaji mengine ya kitaifa,” ameongeza, huku akiipongeza TMA kwa mchango wake endelevu katika kuboresha mifumo ya kuwezesha Biashara Tanzania.

Kwa upande wake meneja wa mradi kutoka ICTPACK, Bw. Renatus Ng’homi, akizungumza alipokuwa akiwasilisha taarifa ya awali ya mradi huo. ameelezea njia ya kiufundi zitakazotumika utekelezaji wa mifumo hiyo, ikiwemo mgawanyo wa rasilimali, na mfumo wa usimamizi wa mradi.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkaazi wa TradeMark Africa Bi. Lilian Masalu amesisitiza dhamira ya shirika hilo katika kurahisisha mchakato wa Biashara kupitia ubunifu wa kidijitali.

“Lengo letu ni kurahisisha biashara. Hii inamaanisha kusaidia taasisi kama FCC kufanya kazi kwa njia ya kidijitali na kwa ufanisi. Tulianza na utafiti wa kina wa utekelezaji, tukachagua ICTPACK kwa ushindani, na tukaunda mradi huu ukiwa na sehemu madhubuti ya kujenga uwezo” 

“Tutaendelea kufuata ratiba tulizojiwekea na kutoa kazi zenye ubora katika kila hatua. Lengo si teknolojia pekee, bali ni kuwa na FCC yenye nguvu zaidi,” amesema.

Ingawa mkataba bado haujasainiwa rasmi, wadau walikutana Jijini Dar es Salaam kwenye kikao cha kimkakati ili kupitia taarifa ya awali ya mradi na kuhakikisha makubaliano kuhusu mfumo wa utekelezaji na ratiba ya mradi.