Home LOCAL ULEGA AWATAKA WAKANDARASI DODOMA RING ROAD KUONGEZA KASI

ULEGA AWATAKA WAKANDARASI DODOMA RING ROAD KUONGEZA KASI

Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amekagua na kuridhishwa na utekelezaji wa ujenzi wa barabara ya mzunguko wa nje ya jiji la Dodoma (km 112.3) ambapo kwa sasa umefikia zaidi ya asilimia 85 ya utekelezaji wake.

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

Ulega ameeleza hayo leo Mei 21, 2025 jijini Dodoma wakati alipokagua hatua za maendeleo ya mradi huo ambapo amewaagiza wataalam wa Wakala wa Barabara (TANROADS) kuhakikisha wanawasimamia Makandarasi wa mradi huo kukamilisha kwa wakati na ubora.

“Nimekagua na nimeridhishwa na hatua zilizofikiwa katika awamu zote mbili na malengo ya Serikali ni kuwa mradi huu ukamilike kwa wakati na nimeelekeza wataalam kutoka TANROADS hadi kufikia mwezi Juni wawe wamefika asilimia 90”, amesisitiza Ulega.

Kuhusu uboreshaji wa miundombinu ya barabara katika jiji la Dodoma Waziri Ulega amesema kuwa Serikali inatarajia kujenga barabara ya njia nne na sita kuanzia Chamwino Ikulu hadi katikati ya jiji hilo ambapo kwa sasa ipo katika hatua za mwisho za manunuzi za kumpata mkandarasi wa kujenga mradi huo.

Ameongeza kuwa katika eneo la Ihumwa Serikali ina mpango wa kujenga barabara ya kisasa ya njia za kupishana (interchange), ili kuruhusu magari kupita katika mji wa Serikali wa Magufuli na yaendayo mjini bila kuwa na kizuizi chochote.

Vilevile, Waziri Ulega amezungumzia umuhimu wa Taasisi za TANROADS, TRC na TPA kufanya kazi kwa kushirikiana ili kuwezesha mradi huo wa kimkakati kukamilika kwa wakati.

Aidha , akiwa katika ziara hiyo Ulega pia alifafanua kuhusu ujenzi wa miundombinu ya barabara za juu (flyovers) katika eneo la Morocco na Mwenge jijini Dar es salaam ambapo amesisitiza kuwa miradi hiyo ipo kwenye mpango mzuri na hatua iliyofikiwa sasa ni kuwa Wizara inaendelea kukamilisha taratibu za kitaalam ili kuendelea na utekelezaji wa miradi hiyo.

Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mkuu na Mkurugenzi wa Barabara kutoka Wizara ya Ujenzi, Mhandisi Aloyce Matei amesema kuwa hadi kufikia mwezi wa saba matarajio yao ni kwamba fedha za mradi wa ujenzi wa barabara za juu za Morocco na Mwenge zitasainiwa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.

Naye, Mkurugenzi wa Miradi kutoka TANROADS, Mhandisi Japheson Nnko amemhakikishia Waziri Ulega kuwa watasimamia Makandarasi hao kuhakikisha mradi wa mzunguko wa nje wa jiji la Dodoma unakamilika kwa ubora na wakati kama ilivyosainiwa kwenye mkataba.

Amebainisha kuwa mradi huo umegawanywa sehemu mbili ambapo Mkandarasi China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) anayejenga sehemu ya Nala-Veyula-Mtumba-Ihumwa bandari kavu (km 52.3) anatarajiwa kukamilisha ifikapo mwezi Julai, 2025 na Mkandarasi Avic International anayejenga sehemu ya Ihumwa bandari kavu-Matumbulu-Nala (km 60) anatarajiwa kukamilisha ifikapo mwezi Agosti, 2025.