▪️Asema ni kutokana na maendeleo yaliyopatikana kipindi cha uongozi wake.
MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama Chama cha Mapinduzi, Waziri Mkuu na Mbunge wa Jimbo la Ruangwa, Kassim Majaliwa amesema kuwa Wilaya hiyo haina deni na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kutokana na kazi kubwa ya kimaendeleo iliyofanyika katika sekta mbalimbali.
Ameyasema hayo leo (Jumamosi, Mei 03, 2025) wakati akizungumza katika kikao kilichojumuisha wajumbe wa Mabaraza ya Jumuia za Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Ruangwa kilichofanyika katika Bwalo Shule ya Awali na Msingi ya Wonder Kids.
Waziri Mkuu amesema kuwa katika kipindi cha kuanzia mwaka 2010 hadi sasa ujenzi wa vituo vya afya umeongezeka kutoka vituo 2 hadi 12 hali inayowezesha kusogeza huduma za afya karibu na wananchi. “Tulikuwa na zahanati 22 lakini sasa zimefikia 35, na jitihada bado zinaendelea.”
Aidha, Waziri Mkuu amesema kuwa kwa kutambua umuhimu wa sekta ya elimu, Wilaya hiyo imewezesha kujenga shule za sekondari 30 kutoka shule 16 za hapo awali.
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa kwa sasa Serikali inatekeleza mradi mkubwa wa maji wa Nyangao – Ruangwa – Nachingwea ambao unajumuisha vijiji 34 vya Wilaya ya Ruangwa, vijiji 21 vya Wilaya ya Nachingwea na unatarajia kunufaisha wakazi 128,657.
Ameongeza kuwa Wilaya hiyo inaendelea na utekelezaji wa ujenzi wa barabara za ndani ya wilaya pamoja na ujenzi wa mradi mkubwa wa ujenzi wa barabara ya Nanganga-Ruangwa ambao upo mbioni kukamilika.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Hassan Ngoma ameipongeza Serikali kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika wilaya hiyo.
Mkuu huyo wa wilaya ametaja baadhi ya miradi kuwa ujenzi wa miundombinu ya barabara, vyumba vya madarasa, maji na vituo vya kutolea hiduma za afya.
Ametumia fursa hiyo kuwasisitiza wakazi wa wilaya hiyo kuendelea kuipa ushirikiano Serikali yao ambayo imejidhatiti kuendelea kuboresha huduma za kijamii.