Ziara ya Tanga na uwekezaji wa Trilioni 3.1
Na: Dk. Reubeni Lumbagala
IMETIMIA miaka minne tangu Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Jemedari wa maendeleo, Dk. Samia Suluhu Hassan, ilipoingia madarakani mwezi Machi 2021. Miaka minne imekuwa ya mafanikio makubwa ikizingatia ajenda ya maendeleo kwa wananchi kama ilivyoelekezwa na Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020-2025, ambayo inasimamiwa kikamilifu ili kujenga ustawi bora wa maisha ya wananchi.
Kimsingi, serikali inao wajibu wa kuwahudumia wananchi wake kwa kuhakikisha inatatua kero zao na kujenga mustakabali mwema wa maisha. Ndiyo maana serikali inakusanya kodi ili iweze kupata uwezo wa kutekeleza mipango ya maendeleo kwa manufaa ya wananchi wake. Utengaji wa fedha za kugharamia miradi ya maendeleo unafanyika kwa umakini mkubwa ili kufanikisha kutimia kwa mipango ya serikali ya kuwahudumia wananchi wake ipasavyo.
Kipekee, niipongeze Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ambayo inatambua umuhimu wa kuwahudumia wananchi wake ipasavyo kwa kuhakikisha inakusanya mapato kutoka kwa wananchi wake ili kuwa na uwezo wa kutekeleza miradi ya kimkakati na ya kimaendeleo kwa maendeleo endelevu. Serikali hii pia imekuwa ikipeleka fedha nyingi kila mkoa na hivyo kufanya mitaa, vitongoji, vijiji, kata na wilaya kushuhudia utekelezaji wa miradi mbalimbali ikigusa sekta za elimu, afya, maji, umeme, barabara, kilimo, viwanda, biashara, uwekezaji, uvuvi na sekta nyingine kadhaa.
Katika miaka hii minne ya Serikali ya Awamu ya Sita, mkoa wa Tanga ni miongoni mwa mikoa ambayo imepata fedha nyingi za miradi ya kimkakati na ya maendeleo. Fedha ambazo mkoa wa Tanga umenufaika nazo zina thamani ya shilingi trilioni 3.1. Kusema kweli, fedha hizi ni nyingi na zimegusa kila sekta muhimu katika maendeleo ya binadamu, na ndiyo maana Rais Dk. Samia Suluhu Hassan alifanya ziara mkoani Tanga kuanzia Februari 23 hadi Machi 1, 2025, kufuatilia thamani ya fedha zilizotekeleza miradi mbalimbali.
Katika siku ya kwanza ya ziara yake akiwa wilayani Handeni, Rais Dk. Samia alisema, “Kuja kwangu Tanga leo ni kuja kuangalia kazi iliyofanywa na fedha hii iliyokuja Tanga trilioni 3.1. Nitatembea na kukagua miradi ya maendeleo ikiwa ya huduma za jamii, miundombinu, kilimo na miradi mingine mingi.” Ni katika siku hiyo ya kwanza ya ziara akiwa wilayani Handeni, Rais Dk. Samia alizindua hospitali ya wilaya ambayo alisema licha ya kuwa hospitali ya wilaya, lakini kwa viwango vyake vya ujenzi, ina hadhi ya kuwa hospitali ya mkoa.
Kwa mujibu wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa, hospitali hiyo imegharimu shilingi bilioni 7.3, huku serikali ikitoa bilioni 4.3 na wadau wa maendeleo, Islamic Help wakitoa bilioni 3. Hospitali hiyo imeshahudumia wagonjwa wapatao 6,846 tangu kuanza kwake na inahudumia wananchi kutoka kata 21 na vijiji 91. Rais Dk. Samia pia aliielekeza TAMISEMI kupeleka shilingi milioni 240 kwa ajili ya kujenga jengo la tiba ya mifupa ili hospitali hiyo iwe maalumu kwa tiba ya mifupa kwa mkoa wa Tanga.
Februari 24, 2025, Rais Dk. Samia aliendelea na ziara yake, ambapo alizindua jengo la Halmashauri ya Bumbuli wilayani Lushoto na kusisitiza litumike vyema kuwahudumia wananchi wanaohitaji huduma. Vilevile, aliweka jiwe la msingi katika mradi wa Bwawa la Umwagiliaji Mkomazi wilayani Korogwe, unaotarajiwa kuhudumia wananchi zaidi ya 20,000 na kuboresha sekta ya kilimo kupitia uzalishaji wa mazao mbalimbali.
Februari 25, 2025, katika Kijiji cha Michungwani wilayani Kilindi, Rais Dk. Samia alifungua Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Tanga. Pia alifungua jengo la Halmashauri ya Mji wa Handeni na kuweka jiwe la msingi la Mradi wa Maji wa Miji 28, ambapo wilaya za Pangani, Korogwe, Handeni na Muheza zinatarajiwa kunufaika na mradi huo kabambe.
Februari 26, 2025, ziara iliendelea wilayani Pangani, ambapo Rais alizindua programu ya ugawaji wa boti kubwa za kisasa 120 pamoja na boti saidizi 118 kwa nchi nzima. Rais Dk. Samia aligawa boti 35 na boti saidizi 60 kwa wavuvi wa Pangani ili kuimarisha sekta ya uvuvi.
Huko Pangani, Rais aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya Bagamoyo (Makurunge) – Pangani – Tanga (Km 256), sehemu ya Mkange – Pangani – Tanga (Km 170.8), pamoja na daraja la Mto Pangani (M525). Ujenzi wa barabara hizi utaunganisha mikoa ya Pwani na Tanga, kuongeza fursa za utalii, biashara na uwekezaji.
Ziara iliendelea Februari 27, 2025, ambapo Rais Dk. Samia aligawa mitungi ya gesi (LPG) wilayani Muheza kwa lengo la kutunza mazingira na afya za wananchi. Pia aliweka jiwe la msingi la Mradi wa Maji Tanga – Horohoro wilayani Mkinga, ambao unatarajiwa kunufaisha wananchi 57,000 kutoka vijiji 37.
Machi 1, 2025, Rais alihitimisha ziara yake mkoani Tanga kwa kutembelea Bandari ya Tanga kujionea maboresho yaliyogharimu bilioni 429.1 na kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa LPG Terminal GBP Gas-Tanga.
Hii ni mifano michache ya miradi iliyoko mkoani Tanga. Kwa hakika, trilioni 3.1 zimeleta maendeleo makubwa mkoani humo katika sekta mbalimbali kama vile afya, maji, umeme, elimu, barabara, kilimo, uvuvi, mifugo, na uwezeshaji wa wananchi kiuchumi. Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Dk. Samia Suluhu Hassan imeonyesha dhamira ya dhati ya kuwaletea wananchi wake maendeleo na ustawi bora wa maisha.
Maoni: 0620 800 462