Home LOCAL WAZIRI SILAA AELEKEZA MINARA YOTE 758 KUWASHWA IFIKAPO 12 MEI 2025

WAZIRI SILAA AELEKEZA MINARA YOTE 758 KUWASHWA IFIKAPO 12 MEI 2025

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

Na Mwandishi Wetu, WMTH, Morogoro

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry William Silaa (Mb), ameelekeza kuwa ifikapo tarehe 12 Mei 2025, saa 6 usiku, ujenzi wa minara ya mawasiliano vijijini uwe umekamilika na minara yote 758 iwe imewashwa, ili wananchi waweze kupata huduma za mawasiliano.

Waziri Silaa alitoa maelekezo hayo tarehe 14 Machi, 2025 wakati wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa minara 758 ya mawasiliano vijijini katika kijiji cha Kidete, Kata ya Chanzuru, Wilayani Kilosa, Mkoani Morogoro.

Rais Samia ametenga kiasi cha fedha Bilioni 126 kwa ajili ya ujenzi wa minara 758 ya mawasiliano vijijini, ambapo kukamilika kwake kutapunguza changamoto ya mawasiliano nchini,” alisema Waziri Silaa.

Ameongeza kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, alizindua Mkakati wa Taifa wa Uchumi wa Kidijitali wa miaka 10, (2024-2034) ambao una nguzo sita, ikiwemo Nguzo ya kuboresha miundombinu ya mawasiliano.

Mnara wa Idete ni moja ya minara iliyopo katika mradi wa minara 758. Mnara huu unajengwa na kampuni ya Airtel, baada ya kupata rukuzu ya serikali, na unatarajiwa kukamilika tarehe 1 Aprili 2025. Huduma zinazotarajiwa kutolewa katika mnara huu ni 2G, 3G, na 4G, hivyo wanakijiji wa kijiji cha Idete na vijiji jirani ndani ya Kata ya Chanzuru wanatarajia kupata huduma hizi mara baada ya mnara huu kukamilika.

Pia, Waziri Silaa alielekeza kuwa mnara huu uwe umewashwa ifikapo tarehe 1 Aprili 2025, na makabidhiano yafanyike tarehe 15 Aprili 2025 kama ilivyopangwa.

Hadi sasa, katika mradi wa Tanzania ya Kidijitali, minara 304 imeongezwa nguvu na imeshakamilika kwa asilimia mia moja. Aidha, katika ujenzi wa minara 758, tayari minara 420 imeshakamilika, ikiwa ni zaidi ya asilimia 55 ya utekelezaji wa mradi huo.

Ujenzi wa minara ya 758 ya mawasiliano vijijini unaotekelezwa na Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) unatarajiwa kunufaisha wananchi wapatao milioni 8.5 waishio vijijini.