Mshauri Mkuu Afrika kutoka Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupunguza Hatari za Maafa (UNDRR) Bwa. Hachim Badji akifafanua jambo katika warsha ya Kuandaa Taarifa ya Nchi ya Utekelezaji wa Mkakati wa Kimataifa wa Sendai (2015-2030) Jijini Dodoma.
Baadhi ya washiriki waliohudhuria warsha wakifuatilia matukio mbalimbali.
Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Meja Jenerali Michael Mmanga akizungumza wakati wa ufunguzi wa Warsha ya Kuandaa Taarifa ya Nchi ya Utekelezaji wa Mkakati wa Kimataifa wa Sendai (2015-2030) Jijini Dodoma.
Mkaguzi Mkuu Usimamizi wa Vihatarishi Wizara ya Fedha na Mipango Bwa. Sako Mayrick akiwasilisha Mkataba wa Sendai kuhusu Maafa na Tanzania katika warsha hiyo.
(PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU
Na: Mwandishi wetu- Dodoma
Serikali imesema itaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo katika mapambano dhidi ya maafa ambayo hujitokeza katika maeneo mbalimbali nchini na kusababisha athari.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Meja Jenerali Michael Mmanga, Jijini Dodoma wakati akifungua Warsha ya Kuandaa Taarifa ya Nchi ya Utekelezaji wa Mkakati wa Kimataifa wa Sendai (2015-2030).
Mkurugenzi huyo alisema uwepo wa mkakati wa Nchi wa upunguzaji wa athari za maafa (2020-2025) na uwezo wa jamii katika kupunguza, kujiandaa na kukabili maafa umeongezeka.
“Nchi yetu imekuwa ikishuhudia kuongezeka kwa matukio ya majanga ambayo yamekuwa yakisababishwa na sababu mbalimbali ikiwemo mabadiliko ya tabia nchi na shughuli za kibinadamu,”alisema Meja Jenerali Mmanga.
Pia aliongeza kwamba pindi maafa yanapotokea husabibisha madhara mbalimbali ikiwemo vifo, majeruhi, upotevu na uharibifu wa mali na miundombinu ya umma iliyotumia gharama kubwa kujengwa.
“Kwa ujumla, majanga haya yamekuwa yakisababisha matokeo hasi katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi kutokana na kupotea kwa mafanikio yaliyopatikana kwa muda mrefu na hivyo, kuzorotesha hatua za maendeleo,”aliongeza.
Aidha kufuatia zoezi la sensa ya watu na makazi inayoendelea nchini Meja Jenerali Mmanga aliwahimiza washiriki wa warsha hiyo kujitokeza kuhesabiwa ili kuiwezesha Serikali kupanga miradi ya maendeleo kwa manufaa ya Taifa.
“Zoezi la sensa linaendelea kwa wale ambao bado hawajahesabiwa hivyo naendelea kuwahamasisha kupata idadi halisi ya watu waliopo nchini itakayowezesha kuandaa rasilimali na mipango halisi inayokidhi mahitaji ya watu nchini,”alihimiza Mkurugenzi huyo.
Naye Mshauri Mkuu Afrika kutoka Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupunguza Hatari za Maafa (UNDRR) Bwa. Hachim Badji aliipongeza serikali kwa kuendelea kuchukua hatua za kukabili maafa pamoja na kushirikisha taasisi mbalimbali.
“Warsha hii itumike kama fursa ya kubadilishana taarifa,uzoefu, mafanikio ambayo tueyapata tagu mwaka 2015 tuweze kujua wapi tulipotoka, tulipo na tunapoelekea katika mapambano haya kama UNDRR tutatoa ushirikiano kufikia malengo yaliyowekwa,” alisema Bwa. Badji.
Kwa upande wake Afisa Mwandamizi Uratibu wa Maafa kutoka Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) Bwa. Juvenal Kisanga alibainisha kuwa WFP imekuwa ikifanya kazi kwa kushirikiana na serikali kuhakikisha maafa yanadhibitiwa na wananchi kufanya shughuli zao katika mazingira salama kwa mujibu wa mpango wa maendeleo endelevu ifikapo 2030.
“UN kupitia wanachama wake waliopo hapa nchini tunafanya kazi kwa kMufuata vipaumbele vya Serikali kwa sababu yenyewe inatengeneza sera, mikakati na mipango ya kupunguza athari za maafa na sisi tunaunga mkono ili kuhakikisha usalama wa wananchi na mali zao,”alieleza Afisa huyo.