Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Wananchi wa Handeni kwenye mkutano wa hadhara katika muendelezo wa ziara yake ya kikazi mkoani Tanga tarehe 25 Februari, 2025.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan mara baada ya kuvuta kitambaa kuashiria uwekaji wa jiwe la mradi wa maji wa Miji 28 kwenye hafla iliyofanyika Handeni Mkoani Tanga tarehe 25 Februari, 2025.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akivuta kitambaa kuashiria ufunguzi wa Jengo la Halmashauri ya Mji Handeni ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya kikazi Mkoani Tanga tarehe 25 Februari, 2025.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amewakumbusha watumishi wa umma kote nchini kuwa wamekasimiwa majukumu ya kuwatumikia wananchi na amewataka wasimame ipasavyo katika nafasi zao na kutimiza majukumu yao.
Rais Dkt. Samia ametoa msisitizo huo leo wakati akizungumza na wananchi na watumishi wa Halmashauri ya Mji wa Handeni mara baada ya kufungua rasmi Jengo la Halmashauri hiyo.
Aidha, Rais Dkt. Samia ameeleza imani yake kuwa jengo hilo linaimarisha utawala bora na huduma kwa wananchi. Jengo hilo ni moja kati ya majengo 122 yaliyojengwa katika Halmashauri mbalimbali nchini tangu mwaka 2021 ikiwemo jengo la Halmshauri ya Wilaya ya Bumbuli ambalo Rais Dkt. Samia amelizindua jana tarehe 24 Februari, 2025.
Awali akiwa Wilaya ya Handeni, Rais Dkt. Samia ameweka Jiwe la Msingi la Mradi wa Maji wa Miji 28 unaoenda kuimarisha upatikanaji wa maji katika Wilaya za Handeni, Korogwe, Muheza na Pangani.
Katika hatua nyingine, akiwa Wilaya ya Kilindi, Rais Dkt. Samia ametambua mchango uliotolewa na marehemu Mhe. Beatrice Shelukindo wakati wa uhai wake katika kutetea haki za wanawake na kupitia nafasi za uongozi alizozishika ikiwemo Ubunge wa Jimbo la Kilindi na Mbunge wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kwa heshima yake, Rais Dkt. Samia ameelekeza Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Mkoa wa Tanga ipewe jina la Beatrice Shelukindo.
Shule hiyo ambayo Rais Dkt. Samia ameizindua leo na inayojikita kwenye masomo ya sayansi ni sehemu ya mpango wa Serikali wa kujenga shule 26 za Wasichana katika kila Mkoa kwa lengo la kuimarisha ushiriki wa wanawake kwenye masomo ya sayansi.
Matukio yote haya ni mwendelezo wa ziara ya wiki moja ya Rais Dkt. Samia katika Mkoa wa Tanga. Pamoja na mambo mengine, jana tarehe 24 Februari 2025, Rais Dkt. Samia aliweka Jiwe la Msingi la Mradi wa Ujenzi wa Bwawa la Umwagiliaji la Mkomazi katika Wilaya ya Korogwe.
Mradi huo unaotarajiwa kuwanufaisha wananchi zaidi ya 20,000 utaimarisha upatikanaji wa maji na kuchochea shughuli za kilimo na uzalishaji wa mazao.
Sharifa B. Nyanga
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu