
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akinywa Kahawa inayozalishwa nchini Tanzania wakati akiwahutubia Viongozi pamoja na wageni mbalimbali kwenye Mkutano wa Tatu wa Nchi zinazozalisha Kahawa Barani Afrika (The 3rd G25 Africa Coffee Summit) uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam tarehe 22 Februari, 2025
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema Afrika inahitaji kurejesha hadhi yake kwenye tasnia ya kahawa duniani.
Aidha, Rais Dkt. Samia amepongeza nchi za Afrika kuja pamoja kujadili uendelezaji wa zao hilo na Umoja wa Afrika kuliingiza zao la kahawa kwenye mazao ya kimkakati, hatua ambazo ni muhimu katika kuanza kurejesha hadhi ya Afrika kwenye tasnia ya kahawa duniani.
Rais Dkt. Samia amesema hayo leo katika Mkutano wa Tatu wa nchi 25 Wazalishaji wa Kahawa Barani Afrika uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC).
Taarifa iliyotolewa na Sharifa B. Nyanga Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu imesema Rais Dkt. Samia pia amesema licha ya tasnia ya kahawa kukabiliwa na changamoto anuwai, bara la Afrika limeanza kupiga hatua katika kukabiliana na changamoto hizo. Aidha, ameeleza imani yake kuwa jukwaa hilo la Nchi Wazalishaji wa Kahawa Barani Afrika litawezesha kuunganisha nguvu katika kukabiliana na changamoto zinazoikumba sekta ya kahawa barani Afrika na kuwa nyenzo sahihi ya kufikia malengo waliojiwekea.
Kwa upande mwingine, Rais Dkt. Samia amezitaka nchi za Afrika ziazimie kuwa ifikapo 2035 nusu ya kahawa inayozalishwa barani Afrika iongezewe thamani barani Afrika kabla ya kuuzwa ndani na nje ya bara hilo.
Akifafanua kuhusu manufaa ya zao la kahawa, Rais Dkt. Samia amesema takwimu zinaonesha kuwa manufaa zaidi ya zao hilo yapo kwenye mnyororo wa thamani mzima kuliko kwenye uzalishaji. Hivyo, Afrika inatahitaji kuwa na viwanda vingi zaidi vya kuchakata kahawa na vya kutengeneza bidhaa nyingine zinatokana na mabaki ya zao hili.
Rais Dkt. Samia amesema kuwa kuendelea kusafirisha kahawa ghafi ni kuendelea kusafirisha ajira za vijana zinazohitajika Afrika, kujikosesha mapato zaidi ambayo yanahitajika kwa maendeleo ya bara la Afrika na kumfanya mkulima wa kahawa aendelee kukosa soko la uhakika wa anachokizalisha.