Home BUSINESS FCS, STANBIC WASAINI MAKUBALIANO KUWAINUA WAJASIRIAMALI MAENEO YA MIPAKANI

FCS, STANBIC WASAINI MAKUBALIANO KUWAINUA WAJASIRIAMALI MAENEO YA MIPAKANI

Mkurugenzi Mtendaji wa The Foundation for Civil Society (FCS)Justice Rutenge, Akizungumza na waandishi wa habari katika hafla ya kutiliana saini makubaliano ya miaka miwili na Benki ya Stanbic Tanzania kupitia taasisi yake ya Stanbic Biashara Incubator, iliyofanyika leo Februari 20, 2025 Jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa Stanbic Biashara Incubator, Kai Mollel (kushoto), akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi kabla ya zoezi la kutiliana saini hati ya makubaliano ya kutekeleza mradi wa miaka miwili unaolenga kuyapa uwezo na kuyainua makundi maalum kibiashara maeneo ya mipakani.

Na; Mwandihi wetu, DSM

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

SHIRIKA la The Foundation For Civil Society (FCS) limeingia makubaliano ya miaka miwili na Benki ya Stanbic Tanzania kupitia kupitia kitengo cha Stanbic biashara incubator unaolenga kuwainua wajasiriamali wanawake na vijana kwa kuwajengea uwezo na kuwapatia ujuzi, maarifa, na fursa za ukuaji wa biashara maeneo ya mipakani.

Akizungumza katika hafla ya kusaini makubaliano hayo yaliyofanyika leo Februari 20, 2025, Jijini Dar es Salaam, MKurugenzi Mtendaji wa FSC Justine Rutenge, amesema makubaliano hayo yana lengo la kuwakwamua kiuchumi wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika kujipatia ajira na kujiinua kiuchumi kwa kuwawezesha kutumia vizuri fursa za masoko ndani na nje ya nchi.

Ameeleza kuwa, FCS inaunga mkono kazi za wajasiriamali zinazofanywa na wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu kulingana na mabadiliko ya FCS kutoka kuwa mfadhili wa ruzuku pekee hadi kuwa mwezeshaji wa maendeleo katika kuchangia uchumi endelevu na shirikishi nchini.

Aidha, Rutenge amebainisha faida za ushirikiano huo kuwezesha wajasiriamali wadogo na wa kati wapatao 350 kuwapa ujuzi na rasilimali, hatua itakayochochea ongezeko la ajira na viwango vya vipato vyao.

“Ushirikiano huu umejikita katika kuimarisha uwezo wa wajasiriamali wanaojihusisha na uchakataji na kuongeza thamani wa mazao ya mboga mboga, matunda na mwani wapatao 350 kupitia programu rasmi za mafunzo. Programu hizi zitazingatia maeneo muhimu kwa mafanikio katika soko la kimataifa, yakiwemo maandalizi ya kuuza bidhaa nje ya nchi, upatikanaji wa fedha za biashara, ujuzi wa kidijitali, na upatikanaji wa masoko.” 

“FCS tunajikita katika kuhakikisha sauti za wananchi zinasikika kwa kushirikiana na sekta za umma na binafsi, tukiyawezesha makundimaalum na jamii nzima kwa ujumla” amesema Rutenge

Ameongeza kuwa mradi huo unafadhiliwa na Trademark Africa (TMA), kwa msaada wa serikali ya uingereza kupitia FCDO, Ireland na Norway.

Kwa upande wake Mkuu wa Stanbic Biashara Incubator, Kai Mollel amesema kuwa lengo la mradi huo ni kuwawezesha wajasiriamali ili biashara zao ziweze kustawi na kuchangia kwa kiasi kikubwa kwenye uchumi wa taifa. 

Mollel, ameleeza kuwa ushirikiano huo  umeandika historia mpya ya vitendo zaidi katika kuhakikisha wajasiriamali wanapata ujuzi, maarifa na fursa za kukuza na kustawisha biashara zao.

“Tunatambua kuwa biashara ndogo na za kati (SMEs) ndizo zinazotoa mchango mkubwa katika ujenzi wa uchumi wa Tanzania. Zinatoa ajira kwa mamilioni ya watu na zina mchango mkubwa katika pato la taifa,”

“Hata hivyo, changamoto bado ni nyingi katika sekta hii, ikiwemo ukosefu wa elimu ya kifedha na mbinu bora za kusimamia biashara, changamoto za mitaji, na upatikanaji wa masoko,” amesema Mollel.

Ameongeza kuwa kwa wafanyabiashara wa mipakani, changamoto ni kubwa zaidi kutokana na vikwazo vya kisheria, ukosefu wa taarifa sahihi na mazingira magumu ya kufanyia biashara, hali inayowafanya washindwe kufanikisha shughuli zao kwa urahisi na ufanisi.

Naye, Meneja Mradi wa FCS Charles Kainkwa amesema Shirika hilo litapeleka wadau wengine kutoa mafunzo mbalimbali ikiwemo jinsi ya kuongeza thamani ya mazao yao na kuwaunganisha na wadau wengine kama BRELA na TBS ili kupata elimu zaidi.

Katika makubaliano hayo FCS na Stanbic watatekeleza miradi miwili kwa pamoja, ikiwemo mradi wa kwanza ukiwahusisha wajasiriamali 100 wa jijini la Dar es salaam na mradi wa pili unawalenga wajasiriamali wanawake pekee wapatao 250 katika mikoa mitano ya mipakani ikiwemo Horohoro jijini Tanga, Namanga jijini Arusha, Holili mkoani Kilimanjaro, Kasumulu jijini Mbeya na Tunduma mkoani Songwe utakaotoa mbinu endelevu za biashara na fursa za upatikanaji wa rasilimali za kifedha na masoko.