…………..
Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amemuapisha Kamishna Mkuu mpya wa Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA), Said Kiondo Athumani. Hafla ya uapisho huo ilifanyika katika Ikulu ya Zanzibar, ikihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali na chama, wakiwemo Makamu wa Pili wa Rais, Hemed Suleiman Abdulla, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk. Mwinyi Talib Haji, Jaji Mkuu wa Zanzibar, Khamis Abdalla Shaaban, Kadhi Mkuu wa Zanzibar, Othman Ngwali, pamoja na viongozi wengine.
Akizungumza mara baada ya kuapishwa, Kamishna Said alimshukuru Rais Dk. Mwinyi kwa imani aliyoonyesha kwake kwa kumteua katika nafasi hiyo muhimu. Alisisitiza kuwa ulipaji kodi ni jukumu la kila mwananchi na kwamba kodi huchangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya kijamii. Aidha, aliahidi kuwa ZRA itaendelea kuwashirikisha walipa kodi kwa njia za uhamasishaji, elimu, na ushawishi ili kuimarisha uhiari wa kulipa kodi.
Kamishna Said alibainisha kuwa zama za kulazimisha ulipaji kodi zimepitwa na wakati, na sasa ni muhimu kushirikiana kwa maelewano na kueleza umuhimu wa kodi kwa maendeleo ya taifa.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Fedha na Mipango, Dk. Saada Mkuya Salum, alisema ZRA imefanikiwa kuvuka malengo ya mapato kufuatia mageuzi makubwa yaliyofanyika. Aliainisha kuwa juhudi za kupambana na ufujaji wa fedha na kuhakikisha uwajibikaji kwa watumishi zimeimarisha ufanisi wa taasisi hiyo, huku mapato yakiwa yameongezeka zaidi ya asilimia 100. Dk. Mkuya alionyesha matumaini kuwa chini ya uongozi wa Kamishna Said, mafanikio zaidi yataendelea kupatikana.
Katika hafla hiyo, aliyekuwa Kaimu Kamishna Mkuu wa ZRA, Said Ali Mohammed, alimkabidhi rasmi ofisi Kamishna Said na kumhakikishia ushirikiano wa dhati katika kuhakikisha malengo ya mamlaka hiyo yanafanikiwa kwa ufanisi zaidi.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa ZRA, Prof. Hamed Rashid Hikmany, alisisitiza umuhimu wa ZRA kama taasisi nyeti kwa maendeleo ya taifa. Alimuomba Kamishna Said kushirikiana kwa karibu na Bodi ya Wakurugenzi ili kufanikisha malengo makubwa ya mamlaka hiyo.
Uteuzi wa Kamishna Said Kiondo Athumani ulifanywa na Rais Dk. Mwinyi mnamo Februari 8, 2025, kufuatia aliyekuwa Kamishna Mkuu wa ZRA, Yussuph Juma Mwenda, kuteuliwa kuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).