Na Mwandishi Wetu
WAKUUWwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Masharii na (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wameazimia kusitishwa mara moja mapigano yanayoendelea Mashariki mwa Congo DRC yanayoendeshwa na Kikosi cha Waasi cha M23 nchini humo.
Maazimio ya Mkutano wa wakuu hao yametolewa katika kikao cha pamoja kilichofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam ambapo viongozi kutoka EAC na SADC walishiriki kuzungumzia hali inayoendelea DRC.
Kutokana na vita hivyo hadi sasa inadaiwa watu zaidi ya 3,000 wamepoteza maisha.
Wakuu hao pia wamesisitiza kutumika kwa njia za Kidemokrasia katika kuendelea kutatua mgogoro huo Mashariki mwa DRC.
Aidha, mkutano huo umeazimia umuhimu wa kuondolewa kwa vikundi vya kigeni, kutokomeza kundi la waasi wa Kihutu, Forces Democratic pour la Libération du Congo (FDLR), linaloendesha shughuli zake Mashariki mwa DRC, pamoja na kuondolewa kwa hatua za ulinzi za Rwanda na vikosi vya Rwanda kujiondoa nchini humo.
Vile vile mkutano huo umewaagiza wakuu wa majeshi kutoka nchi wanachama wa EAC na SADC, kukutana ndani ya siku tano na kuandaa mpango wa usalama wa Goma na maeneo jirani, sambamba na kujadili ufunguzi wa uwanja wa Ndege wa Goma na njia kuu za usafirishaji na kuwezesha usambazaji wa misaada ya kibinadamu mashariki mwa nchi hiyo.
Pia wakuu hao wamempongeza na kumshukuru Rais Dkt. Samia kwa kukubali kuwa mwenyeji wa mkutano huo uliopelekea kutoa maazimio ya kuikomboa Jamhuri ya Congo.