Home LOCAL WASIRA ATAKA VIKAO CCM VIJADILI SHIDA ZA WATU

WASIRA ATAKA VIKAO CCM VIJADILI SHIDA ZA WATU

Na; Mwandishi Wetu, Bunda
 
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira, ameagiza vikao vya Chama kuzungumza mambo yanayowahusu wananchi kwa lengo la kusikia changamoto zao na kuwa sehemu ya kupatiwa ufumbuzi.
 
Amesisitiza kuwa siyo sahihi vikao hivyo kujadili mambo yasiyo na maana wakati wananchi kjatika maeneo husika wanakabiliwa na changamoto ambazo endapo zitasikilizwa na kufikishwa mbele ya mamlaka husika zitapatiwa ufumbuzi.
 
Wasira alieleza hayo jana alipokutana na kuzungumza na wafanyabiashara na wajasiriamali wa Wilaya ya Bunda mkoani Mara, mjini Bunda, jana.
 
“CCM ni lazima isikilize watu wanataka nini, sisi ni Chama cha watu na kwa kweli tunataka kiwe cha watu kwelikweli, vikao vyetu vya CCM vizungumze mambo ya watu, kama ni mambo ya wafanyabiashara wadogowadogo (machinga) tuzungumze kuhusu hilo, kama wana matatizo wakimbilie CCM kwa sababu wanajua huko ndiko kuna usalama.
 
“Kuna akina mama siku moja walinipigia simu wakanieleza kuwa wanafukuzwa barabarani nikauliza mlikuwa mnafanya nini, wakasema walikuwa wanafanyabiashara, nikawaambia nendeni kwa DC (Mkuu wa Wilaya) wakasema DC hatujamuona, nikawaambia nendeniiCCM kwa katibu wa wilaya, mwambieni atumie simu yake amwambie DC wakae pamoja wawasikilize. Hatuwezi kuendesha nchi bila ya kusikiliza watu.” alisema.
 
Makamu Mwenhyekiti Wasira alisema kuwa, ni vema vikao vianze kusikiliza machungu hyanayowagusa wananchi ili kupata ufumbuzi wa changamoto zao mbalimbali.
 
“Unajua vikao hivi wakati mwingine mnajikuta mnajizungumza wenyewe badala ya kuzungumza wafanyabiasha wana matatizo gani, mama lishe wana matatizo gani, wakulima wana matatizo gani,” alisema.
 
TUTAENDELEZA USHIRIKIANO SEKTA BINAFSI
 
Wasira alisema serikali inazoziongoza zitaendelea kuimarisha uhusiano na ushirikiano na sekta binafsi kwa nia ya kuchochea maendeleo ya wananchi na upatikanaji wa huduma bora.
 
“Huko nyuma tulikuwa tunatumia zaidi serikali, lakini dunia imebadilika sana hatuwezi kutumia mitaji ya serikali, kwa hiyo tumegawana biashara ifanywe na sekta binafsi, mambo yanayohusu umma kwa ujumla kama barabara, elimu, ingawa watu wengine wanawekeza shuleni na wanapata faida lakini ni haki ya watu wote, ukiuza wasiokuwa na hela hawataipata, lakini katika kuzalisha mali, kusambaza mali ambapo vyote hivyo vinakuza uchumi tunaikaribisha sekta binafsi, hapo ndipo tunapogawana kazi, lakini tunahusiana,” alisema.
 
“Mimi leo nimekuja kuzungumza na nyie wafanyabiashara na nimekuja kuzungumza na nyie kwa ajili ya kufanya kazi ya Chama Cha Mapinduzi ya kuboresha maisha ya wananchi, huwezi kuboresha maisha bila ya kusikiliza maana katika dunia hii maisha yana vikwazo, ukisikiliza utajua kwamba ukiondoa kikwazo hiki mambo ya kukuza uchumi yatakwenda kwa ‘speed’ (kwa kasi) na maisha yatakwenda.
 
Alisema ingawa CCM ni Chama cha siasa na siyo serikali, lakini Chama ndicho kinaongoza serikali na kazi yake ni kuwasikiliza wananchi ili kuiambia serikali kwamba matatizo ya wananchi ni nini.

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!