Dar es Salaam, 24 Januari, 2025
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amemtaka Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), Yusuph Mwenda kusimamia usawa katika kulipa kodi.
Rais Dkt. Samia ametoa tamko hilo leo wakati wa hafla ya utoaji tuzo za shukrani kwa Mlipakodi Bora wa mwaka 2023/24 zilizotolewa na TRA katika ukumbi wa The Super Dome Masaki.
Aidha, Rais Dkt. Samia amemtaka Kamishna huyo kuchukua hatua za haraka kwa watumishi wanaotengeneza mazingira ya kutokuwa na usawa katika ulipaji wa kodi na yanayochochea rushwa.
Vile vile, Rais Dkt. Samia amemuelekeza kuchunguza mienendo ya watumishi na kuchukua hatua za haraka na bila upendeleo kwa mtumishi yeyote anayejihusisha na vitendo vya rushwa ikiwemo kusaidia ukwepaji kodi.
Rais Dkt. Samia amesema ukwepaji kodi unaathiri wananchi, wafanyabiashara na nchi kwa ujumla, kusababisha kuchelewesha maendeleo ya nchi na kuifanya Serikali kushindwa kutekeleza mipango yake ya maendeleo kwa wakati kama ilivyokusudiwa.
Kwa upande mwingine, Rais Dkt. Samia amesema dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ni kuendelea kujenga mazingira wezeshi ya watu kufanya kazi, biashara na uchumi kuendelea kukua, ili Serikali ipate kodi kwa ajili ya kuendelea kuboresha huduma za jamii na ustawi wa watu.
Hali kadhalika, Rais Dkt. Samia ameongeza kuwa kwa kuzingatia dhamira hiyo ya Serikali, mwaka 2024 aliunda Tume ya Maboresho ya Kodi nchini ili ifanye tathmini ya mfumo wa kodi na kuleta mapendekezo ya namna ya kuboresha mfumo wa kodi nchini.
Lengo la Tume hiyo ni kujenga mfumo wa kodi unaoimarisha usawa katika kulipa kodi, unaotabirika, ulio rahisi na usio na usumbufu na wenye viwango vya kodi rafiki.
Rais Dkt. Samia pia amesema Serikali imedhamiria kuwa na mfumo wa kodi unaorahisisha na kuchagiza shughuli za kiuchumi ili kodi ikusanywe kwa wingi, kuleta maendeleo kwa haraka zaidi na kupunguza utegemezi wa kibajeti.
Kuhusu matumizi ya TEHAMA, Rais Dkt. Samia ameitaka TRA kutumia mifumo hiyo katika kumhudumia kwa wakati mlipa kodi wa mwisho na kuongeza mapato ya kikodi yanayoendana na uwekezaji uliofanywa katika kujenga uchumi wa kidijitali na kuwarahisishia walipa kodi kutimiza wajibu wao.
Sharifa B. Nyanga
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu