Marehemu Winjuka Songalaeli Mkumbo enzi za uhai wake.
Madiwa hao wakiwa tayari kwa ajili ya ibada hiyo iliyoongozwa na Askofu wa Kanisa la Assemblies of God Singida Kaskazini, Noel Lameck.
Askofu Noel Lameck akiongoza ibada hiyo.
Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dorothy Mwaluko, akitoa salama za rambirambi za mkoa.
Na: Dotto Mwaibale, Singida
AJALI ya Basi la Tanzanite lenye namba za usajili T 916 DNU iliyoua watu tano mkoani Singida imeibua mapya baada ya mmoja wa mashuhuda wa ajali hiyo kueleza kuwa mabasi yanayofanya safari kati ya Mwanza, Dodoma na Dar es Salaam madereva wamekuwa wakishindana kufika mapema kwa kuchochewa na bonasi inayotolewa na matajiri wa magari hayo.
Hayo yalibainishwa na Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara Wanawake Mkoa wa Singida, Prisca Maleta anayeishi Manyoni mkoani hapa ambaye alikuwa mtu wa kwanza kushuhudia ajali hiyo na kutoa msaada kwa majeruhu na kuzistiri maiti.
Maleta aliyasema hayo jana kwenye ibada ya mazishi ya Diwani Viti Maalum wa Tarafa ya Kinampanda Wilaya ya Iramba Winjuka Mkumbo ambaye alikuwa ni miongoni ya watu waliopoteza maisha katika ajali hiyo.
“Mimi ni Mwanaharakati nilifuatilia jambo ili na nilipoongea na Winjuka eneo la ajali aliniaambia mwendo wa basi hilo tangu linaondoka Singida ulikuwa mbaya kwani dereva alikuwa akiendesha kwa kasi na kusababisha abiria kuanza kutafutana na walipofika Manyoni abiria walimkataa na akaanza kuendesha dereva mwingine wa akiba ambaye naye alikuwa akiendesha kwa mwendo wa kasi kuliko yule wa mwanzo hadi tairi lilipopasuka na kusababisha ajali” alisema Maleta.
Alisema alipofuatilia kwa karibu aligundua sababu ya mwendo kasi wa mabasi hayo ni madereva hasa wa mabasi ya kutoka Mwanza kugombea mnara yaani anayekuwa wa kwanza kufika anapewa bonasi na matajiri wa mabasi hayo.
“Tunaomba Serikali kuliangalia jambo ili kwani matajiri wengi wanawapatia madereva wao minara na wa kwanza kufika ndiye atakayepewa bonasi na suala la pili ni wale watu wanaofika eneo la ajali tukiwaamini kwa asilimia 100 ndio wanakuwa wa kwanza kuwafilisi kwa kuwaibia majeruhi na watu waliopoteza maisha kwani nimewashuhudia kwa macho yangu na wanangu wakiwafunua zile nguo zetu tulizowa wasitiri kwa kuwafunika na kuanza kuingiza katika mifuko yao na kuchukua fedha na vitu vingine vya thamani kwa kuwa tunawafahamu baadhi yao majina tumempa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Manyoni kwa
ajili ya kushughulikia suala hilo” alisema Maleta.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida, Alhajj Juma Killimbah alisema Rais Samia Suluhu Hassan ametoa fedha nyingi kwa ajili ya kujenga vituo vya afya, zahanati na Hospitali lengo likiwa ni kuwasaidia wananchi pale wanapokuwa wagonjwa na kupata ajali lakini amesikitishwa na kitendo cha majeruhi wa ajali hiyo kuona wakipoteza maisha licha ya kuwepo huduma za hospitali karibu na eneo la ajali.
“Ajali imetokea mlima Saranda, pale Kintinku pana zahanati,Maweni pana Kituo cha afya na Manyoni pana Hospitali ya wilaya ni umbali wa kilomita zisizozidi 20 kwa nini hawa majeruhi wasingepelekwa katika maeneo hayo kwa ajili ya kupata huduma ya kwanza ambayo ingesaidia kuzuia damu zisitoke badala yake wakawachukua na kuwapeleka Dodoma umbali wa zaidi ya kilometa 150 bila usaidizi wowote na baadhi yao kujikuta wakipoteza maisha akiwepo diwani Winjuka” alisema Killimbah.
Killimbah alitumia nafasi hiyo kutoa agizo kwa Serikali kuhakikisha inaaliangalia jambo hilo kwa karibu na kuwa itakuwa haina maana kuwa na zahanati, vituo vya afya, hospitali kila mahali lakini wananchi wanapoteza maisha kwa kuwasafirisha umbali mrefu kwa ajili ya kuwapatia matibabu huku wakikosa huduma kwenye maeneo ya karibu ambazo zingesaidia kuokoa maisha yao.
Katika mazishi hayo simanzi na vilio na watu kuzimia vilitawala huku kila
mtu akimzungumzia marehemu Winjuka Mkumbo kwa jinsi alivyokuwa akijitoa
kusaidia jamii katika Wilaya ya Iramba na maeneo mengine ya jirani.
Akiongoza ibada ya mazishi Askofu Noel Lameck wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God Singida Kaskazini alisema umati wa watu uliokuwepo katika ibada hiyo unaonesha jinsi Winjuka Mkumbo alivyokuwa akiishi vizuri na jamii na kanisa na akatumia ibada hiyo kumuomba kila mtu kujiandaa kwa kutubu na kuokoka.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Iramba Michael Matomora akitoa salamu za rambimbia aliagiza kila siku kuhakikisha gari lake linakuwa limewekwa mafuta  ili kusaidia kusafiri wakati wote hasa kunapokuwepo na jambo la dharura.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Innocent Msengi alisema halmashauri hiyo tangu itokee ajali hiyo na kumpoteza diwani wao Winjuka Mkumbo imetoa ushirikiano na kugharamia mambo mbalimbali yaliyokuwa yakihitajika.
Miongoni waliopata fursa ya kumzungumzia marehemu Winjuka ni pamoja na Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dorothy Mwaluko ambaye alitoa rambirambi kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mbunge wa Iramba Magharibi ambaye pia ni Waziri wa Fedha na Uchumi , Dk.Mwigulu Nchemba, Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Singida, Martha Gwau, Wajumbe wa Kamati ya Siasa kutoka wilaya ya Iramba na Mkoa wa Singida wakiwepo, Diana Chilolo, Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa, Ahmed Kaburu.
Makundi mengine yaliyopata fursa ya kutoa rambirambi zao na kumzungumzia marehemu Winjuka ni vikundi vya wananawake vilivyokuwa vikisaidiwa na marehemu, wanafunzi zaidi ya 900 waliokuwa wakisomeshwa na kusaidiwa na marehemu kupitia Shirika la Ndugu la Sweden, watu binafsi, makanisa mbalimbali na taasisi zingine zilizopo wilayani humo.
Marehemu Winjuka Songalieli Mkumbo alizaliwa tarehe Oktoba 6, 1974 katika Kijiji cha Simbalugwala ambapo alihitimu darasa la saba mwaka 1989 na kufunga ndoa na John Lyanga katika Kanisa la T.A.G Mwaka 1991.
Enzi za uhai wake marehemu ameshika nyazifa mbalimbali katika kanisa na maeneo mengine na hadi anafariki alikuwa Diwani wa Viti Maalum wa Tarafa ya
Kinampanda wilayani Iramba mkoani Singida.
Marehemu Winjuka Mkumbo alifariki Agosti 17, 2022 kwa ajili ya gari iliyotekea Mlima Saranda wilayani Manyoni na ameacha mme, watoto watatu, wawili wa kike na wakiume mmoja Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi amen.Â
Â