Na. WAF – Dar es Salaam
Mkutano wa ushauri wa kitaalamu wa kutokomeza ugonjwa wa USUBI nchini umemalizika kwa kukubaliana na kushauriana mbinu zitakazo wezesha kutokomeza ugonjwa huo ifikapo mwaka 2030.
Mkurugenzi msaidizi – Epidemiolojia kutoka Wizara ya Afya Dkt. Azma Simba amesema hayo mara baada ya kufunga mkutano huo uliofanyika jijini Dar es Salaam kwa kuhusisha Wataalamu mbalimbali kutoka Tanzania na nje ya nchi.
Miongoni mwa mambo waliyokubaliana katika kikao hicho ni pamoja na kuendeleza juhudi za kumezesha kinga tiba pamoja na utoaji wa elimu kwa jamii ili kufikia lengo la mwaka 2030.
Dkt. Simba amebainisha kuwa Ugonjwa wa USUBI unaathiri ngozi ya binadamu, kupatwa na homa kali, kutokwa na vipele mwilini, kuhisi uwasho mkali pia unaweza kusababisha upofu.
“Ugonjwa huu huenezwa na nzi wadogo weusi ambao kitaalamu wanaitwa (blackfriars) pia huzaliana katika maeneo yenye misitu na maji yanayotiririka kwa kasi.” Amesema Dkt. Simba
Aidha, ugonjwa huo wa USUBI umeenea katika Halmashauri 29 ambapo takribani 7.02% ya watu wapo katika hatari ya maambukizi ya ugonjwa huu nchini.
Hata hivyo, Dkt. Simba amesema mikakati mbalimbali inafanyika hapa nchini ikiwemo kumezesha kinga tiba kwa maeneo mengine ni mara moja kwa mwaka huku maeneo mengine wanamezesha mara mbili kwa mwaka.
“Juhudi zilizofanyika hadi sasa kupitia programu maalumu ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ni pamoja na kuainisha maeneo yaliyoathirika na ugonjwa huu kwa kufanya tafiti na tathmini katika maeneo hayo kwa kushirikiana na wadau (NIMR, MUHAS, TFGH, CDC, WHO, KCMC, USAID, RTI).” Amesema Dkt. Simba.
Mwisho, Dkt. Azma Simba amewataka wananchi kuunga juhudi hizo zinazofanywa na Serikali ili kutimiza azma yake ifikapo mwaka 2030 kutokomeza ugonjwa huu wa USIKU.
Ikumbukwe kuwa hizi ni juhudi ambazo zinaendelea kufanywa baada ya agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. @samia_suluhu_hassan kusaini azimio la Kigali mnamo 27, Januari 2022 lengo ikiwa ni kujitoa kwa 100% kuhakikisha Tanzania inatokomeza Magonjwa ya kitropiki yaliyokuwa hayapewi kipaumbele (NTDs) ifikapo 2030.