Home LOCAL WAZIRI CHANA AMUAPISHA KAMISHNA UHIFADHI NCAA, AMPA MAAGIZO MAZITO

WAZIRI CHANA AMUAPISHA KAMISHNA UHIFADHI NCAA, AMPA MAAGIZO MAZITO

Na Happiness Shayo- Karatu

Waziri wa Maliasili na Utalii ,Mhe. Balozi Dkt. Pindi Hazara Chana amemuapisha na kumvisha cheo cha kijeshi Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, CC Dkt. Elirehema Joshua Doriye huku akimtaka kuitumia nafasi hiyo kuonesha utendaji uliotukuka na wenye tija kwa maslahi ya Watanzania wote.

Hayo yamejiri katika hafla ya kuvishwa cheo na kuapishwa kwa Kamishna Doriye iliyofanyika Makao Makuu ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro leo Desemba 23,2024.

“Ni matumaini yetu makubwa kuwa utaendelea kutumia vipawa vyako kuhakikisha mafanikio makubwa yanapatikana katika mamlaka hii, hususani katika kipindi hiki ambacho sekta ya utalii inaendelea kushamiri duniani. Katika kipindi kifupi cha utendaji wako, tumeona mafanikio makubwa yanayodhihirisha uwezo wako” amesisitiza Mhe. Chana.

Aidha, Mhe. Chana amemuelekeza Kamishna Doriye kuhakikisha Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro inapanua Wigo wa Utalii kwa kuweka mipango ya kuboresha vivutio kama Olduvai Gorge, Mapango ya Amboni, Kimondo cha Mbozi, magofu ya engaruka na eneo la mumba ili kuvutia watalii zaidi katika vivutio hivi vya mambo kale.

Pia, ameitaka Mamlaka ya NCAA kuimarisha Miundombinu kwa kuhakikisha miundombinu ya utalii inaboreshwa ili kutoa huduma bora kwa watalii wanaotembelea vivutio vyetu na pia kuhakikisha barabara zinapitika muda wote sambamba na kuimarisha mahusiano ya kikazi kati ya watumishi na wadau wengine nje ya mamlaka ili kuboresha utendaji.

Naye, Kamishna Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Dkt. Elirehema Doriye ametumia fursa hiyo kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumteua katika wadhifa huo huku akiahidi kuitumikia nafasi hiyo kwa uwajibikaji wa hali ya juu.

“Dhamira yangu ni kusimamia uhifadhi endelevu wa Hifadhi ya Ngorongoro, nitahakikisha rasilimali za kiasili na kihistoria zinalindwa dhidi ya uharibifu sambamba na kuongeza matumizi ya teknolojia katika utendaji kazi” Dkt. Doriye amesema.

Dkt. Doriye ameongeza kuwa atahakikisha anakuza utalii wa kimkakati kwa kuimarisha miundombinu, huduma na ubora wa vivutio vya eneo la Ngorongoro, kuimarisha ushirikiano ndani ya taasisi na jamii katika kubuni na kutekeleza mipango ya mamlaka hiyo na kuboresha maslahi ya wafanyakazi.

Kwa upande Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi ameahidi kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii itahakikisha inatoa ushirikiano wa kutosha kuhakikisha mipango na malengo ya mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro yanafikiwa.

Hafla hiyo imehudhuriwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula,Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Arusha,Manaibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Mwenyekiti wa Bodi ya NCAA, Jenerali Venance Mabeyo (Mstaafu),Wakuu wa Wilaya za Karatu na Ngorongoro, Wenyeviti wa CCM Karatu na Ngorongoro, Wakurugenzi wa Bodi ya NCAA,Menejimenti ya Wizara ya Maliasili na Utalii,Mkurugenzi Kitengo Cha Uratibu wa Jeshi la Uhifadhi, Wakuu wa Taasisi zilizoko chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii,Wakurugenzi wa Halmashauri za Karatu na Ngorongoro, Menejimenti ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro naMaafisa na Askari wa NCAA.

http://WAZIRI CHANA AMUAPISHA KAMISHNA UHIFADHI NCAA, AMPA MAAGIZO MAZITO

Previous articleHAYA HAPA MAGAZETI YA LEO JUMATATU TAREHE 23,DISEMBA 2024.
Next articleGRIDI ZA TANZANIA NA KENYA KUIMARISHA UPATIKANAJI WA UMEME NCHINI – MHA. GISSIMA NYAMO-HANGA

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here